Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere - Mara

ZIARA YA WAZIRI UMMY NA LUKUVI KUWEKA MSUKUMO UJENZI WA HOSPITALI YA MWALIMU NYERERE

Posted on: March 5th, 2020

Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto  Ummy Mwalimu ameridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa  Hospitali ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere - Nkwangwa (MWALIMU NYERERE MEMORIAL  MEDICAL CENTER) kwani ujenzi wake unaenda vizuri kwa kufuata vigezo na viwango vya utendaji kazi wa Serikali ya awamu ya tano.

Waziri Ummy amesema hayo Leo alipotembelea Hospitali hiyo akiambatana na Waziri wa Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi .Lengo la ziara hiyo ilikua ni kukagua maendeleo ya ujenzi wa Hospitali hiyo pamoja na kuweka msukumo wa kuhakikisha kwamba hospitali hiyo ya rufaa ya kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere inakamilika kwa wakati kwa sababu wananchi wa mkoa wa Mara wameisubiri kwa muda mrefu.

 Ameongeza kusema kuwa Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii ,Jinsia, Wazee na Watoto  inataraji kuwa Hospitali hii haitaishia tu kuwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara itakayohudumia watu zaidi ya Million 2.3 wa Mkoa wa Mara, bali itakuwa hospitali ya Rufaa yenye kutoa huduma za kibingwa na bobezi kwa kanda ya ziwa.

Akizungumza katika ziara hiyo,Waziri Ummy amelipongeza shirika la nyumba la Taifa (NHC) kwa kazi nzuri wanayoifanya na kuwataka kufanya kazi usiku na mchana ili kuhakikisha wanakamilisha ujenzi huo kwa muda uliokusudiwa na  Hospitali ya Rufaa  ya Mkoa wa Mara iweze kuhamia mahali hapo  na kuanza kutoa huduma kwa wananchi.

Nae Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe.William Lukuvi amewahakikishia wananchi wa Mkoa wa Mara kuwa ujenzi wa hospitali hiyo utakamilika kwa wakati maana lengo la ujio wao ni kuja kutatua changamoto zilizokuwa zinasababisha ucheleweshaji wa kukamilika kwa jengo hilo. Pia amesema kuwa Chuo kikuu cha Adhi wanaendelea kuwepo site kusimamia na kuhakikisha ujenzi unakamilika kwa wakati na wa kiwango maana Serikali ya Awamu ya tano inaenda kwa viwango na thamani ya pesa(value for money).

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Adam Malima amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. John Pombe Magufuli kwa kukubali kutoa pesa takribani billion 15 kwa ajili ya kumalizia ujenzi wa hospitali hiyo ambao ulisimama kwa Zaidi ya miaka arobaini. Pia amewashukuru Mawaziri wote kukubali kuja na kukaa pamoja kuona jinsi gani wanaweza kufanya ili kukwamua changamoto ambazo zilikuwa zinasababisha kuchelewa   kukamilika kwa ujenzi huo. Hivyo amesema kuwa wanatarajia ifikapo katikati ya mwezi wa nne wananchi wa Mkoa wa Mara wataanza kupata huduma za Mama na Mtoto katika hospitali hiyo na ifikapo tarehe 1 Julai Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara inaweza kuhamia mahali hapo.

Tazama hapa >>>