Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere - Mara

HUDUMA ZA MATIBABU KUANZA KUTOLEWA HOSPITALI YA MWL. NYERERE - KWANGWAGWA

Posted on: August 14th, 2020

Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia ,Wazee na Watoto Mh.Ummy Mwalimu ameridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa Hospitali ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere –Kwangwa na kumtaka Mkandarasi wa mradi huo kuongeza kasi kukamilisha ujenzi  ili ndani ya wiki mbili kuanzia sasa huduma za Afya zianze kutolewa katika hospitali hiyo.

Mhe.Ummy amesema hayo leo alipotembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa hospitali hiyo ambapo amepongeza juhudi zinazofanyika kuhakikisha hospitali hiyo inakamilika kwa wakati ili kiu ya wananchi wa Mkoa wa Mara  kupata huduma bora za Afya ipate kutimia maana wamesubiri kwa muda mrefu takribani miaka arobaini  kukamilika kwa jengo hilo na kuanza kutoa huduma.

“Tarehe ya ufunguzi wa jengo hili haitasogezwa mbele na ninakutaka Mganga Mfawidhi wa hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara Dr.Joachim Eyembe pamoja na timu yako mjipange na kuhakikisha mnaanza kutoa huduma ili pindi nitakaporudi kufungua jengo hili nikute huduma tayari zimekwishaanza kutolewa.”

Katika hatua nyingine Waziri Ummy amesikitishwa na kutoridhishwa na utendaji kazi wa Mshauri Mwelekezi wa mradi huu ambae ni Chuo Kikuu cha Ardhi na kumuagiza Makamo Mkuu wa Chuo hicho Prof.Evarist Lawi kufanya mabadiliko ya msimamizi mshauri kutokana na utendaji kazi wake duni na kusema kuwa alidhamiria kuvunja mkataba lakini amebadili maamuzi baada ya kuona kuwa Chuo cha Ardhi wanafanya kazi nzuri sana katika miradi mingine ya kimkakati ya wizara hivyo kusuasua kwa mradi huu yawezekana ni mapungufu  binafsi ya msimamizi.

Aidha mh. Ummy alisema kuwa sambamba na huduma zitakazotolewa,Pia huduma ya usafishaji figo inaanza rasmi kutolewa katika hospitali hiyo jambo ambalo litapunguza gharama na kusaidia wananchi wanaoifuta huduma hiyo katika hospitali zingine nje ya Mkoa sasa kuanza kuzipata ndani ya Mkoa hivyo wananchi wanashauriwa kukata Bima za Afya ili kupunguza gharama za matibabu maana matibabu ya kusafisha figo yana gharama kubwa.

Aliongeza kusema kuwa ,kuboreka kwa huduma za kibigwa isiwe sababu ya wananchi kusahau kuendelea kuchukua hatua za kujikinga na maambukizi ya Corona pamoja na magonjwa yasiyo ya kuambukizwa badala yake  ameshauri wananchi kuendelea kuchukua tahadhari kwa kunawa mikono,kula vyakula vinavyofaa,kuepuka unywaji wa pombe na uvutaji sigara uliokithiri pamoja na kufanya mazoezi angalau dakika 30 mara tatu kwa wiki.

Awali akimkaribisha Waziri wa Afya,Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe.Adam Kighoma Malima amemuomba Waziri wa Afya kutatua changamoto na kuondoa tofauti  iliyopo baina ya Mashauri mwelekezi pamoja na mkandarasi wa mradi ambaye ni Shirika la Nyumba la Taifa(NHC) ili  Kiu na matamanio ya Mkoa kuona hospitali hii inakamilika na kuanza kutoa huduma  ndani ya kipindi cha kwanza cha Uongozi wa Rais  John Pombe Mgufuli inatimia sababu ni jambo linaloonesha kuunga mkono juhudi za Rais katika kuhakikisha huduma za Afya kwa wananchi zinaboreshwa.

“Mhe.Rais John Pombe Magufuli ameikwamua hospitali hii ambayo ujenzi wake ulisimama takribani  Zaidi ya miaka arobaini kwa kutoa Billion 15 ili kukamilisha ujenzi huu,hivyo ni jambo la kusikitisha kuona watu wanakwamisha ujenzi huu kwa matakwa yao binafsi pasipo kujali maslahi ya wannchi wanaohitaji huduma hii.Waziri naomba nisaidie Mkandarasi pamoja na Mshauri mwelekezi wakae chini na kutatua tofauti zao ili ujenzi uendelee na kukamilika kwa wakati uliokusudiwa.

Sambamba na hayo Waziri Ummy ametoa pongezi kwa Mkoa wa Mara kusimamia ipasavyo utoajia wa huduma bora za Afya ambapo amesema katika tathmini ya miaka mitano ya uongozi wa  Serikali ya Awamu ya Tano Huduma za Afya katika Mkoa wa Mara Zimeboreshwa sana kwa kuwa na uwekezaji  unaogusa maisha ya watanzania,kuongezeka kwa idadi ya hospitali na vituo vya afya,upatikanaji wa dawa na vifaa tiba pamoja kuwepo kwa  madaktari wa kutosha kuhudumia wananchi.