WAZIRI MKUU ARIDHISHWA NA MAENDELEO YA UJENZI WA HOSPITALI YA MWALIMU NYERERE KWANGWA
Posted on: December 5th, 2019Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa amepongeza uongozi wa serikali ya mkoa wa Mara pamoja na Uongozi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara chini ya usimamizi wa Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo Dr .Joachim Eyembe kupitia Wizara ya Afya, maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ,kwa maendeleo mazuri ya ujenzi wa HospitalI ya Mwalimu Nyerere Kwangwa, iliyoanza kujengwa na Baba wa Taifa Mwl. Julius Kambarage Nyerere takribani miaka arobaini(40) iliyopita.
Mh. Waziri Mkuu amesema hayo mapema leo alipokuwa katika ziara yake ya kutembelea miradi mikubwa ya maendeleo Mkoani Mara na kumlazimu kutembelea hospitali hiyo ili kufuatilia maendeleo ya ujenzi Hospitali hiyo unaogharimu takribani billioni kumi na tano(15). Katika ziara hiyo amekagua na kufurahishwa na kazi kubwa na nzuri inayofanywa na shirika la nyumba la Taifa (NHC), chini ya Mkurugenzi wa shirika hilo Dr. Maulid Banyani.
Licha ya pongezi hizo, amemuhakikishia Mkurugenzi huyo kuwa fedha zipo, hivyo wanatakiwa kufanya kazi usiku na mchana ili kuhakikisha ujenzi huo unakamilika hata kabla ya muda uliopangwa.
Amesema, “jengeni usiku na mchana jengo hili wananchi hawa wanasubiri wamechoka kuliona likiwa halifanyiwi kazi,wanataka sasa kuona jengo hili limejengwa kwa ajili ya nini?ili waje watibiwe”.
Waziri Mkuu ameendelea kusema kuwa Hospitali hii ni kubwa ya kimkakati katika kanda ya Ziwa ambapo itakuwa na maeneo makuu matatu, eneo la kwanza “wing C” litakua eneo la kutibia akina mama na watoto, eneo la kati “Wing B” litakua Hospitali ya Mkoa na eneo la mwisho litakua kitengo cha mifupa ambapo amesema kitengo cha mifupa kitakuwa kitengo cha pili kwa ukubwa kutoka kile cha Muhimbili MOI. Hivyo kukamilika kwa ujenzi wa Hospitali hiyo kutafungua fursa za kibiashara ikiwemo kutibu wagonjwa toka nchi Jirani ya Kenya.
Mbali na hayo amewashukuru wananchi wa mkoa wa Mara kuendelea kuunga mkono juhudi za maendeleo zinazofanywa na serikali ya Rais John Pombe Magufuli na kuahidi kuwa serikali haitawaangusha. Pia ametumia nafasi hiyo kuwakaribisha wananchi wa Mkoa wa Mara kushiriki katika maadhimisho ya sherehe ya uhuru ambayo kitaifa yanatarajiwa kufanyikia jijini Mwanza tarehe 9.12.2019 na mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr.John Joseph Pombe Magufuli
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mara Mh.Adam Malima kwa niaba ya wananchi wa mkoa wa Mara amemshukuru Waziri Mkuu kwa kumtaja kuwa kinara wa maendeleo ya mkoa wa Mara kwa jitihada zake za kufanikisha upatikanaji wa fedha za kumalizia ujenzi wa wa Hospitali hiyo. Aidha amemshukuru Rais Wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. John Pombe Magufuli kwa kusikia kilio cha wananchi wa Mara na kukubali kutoa fedha Zaidi ya bilioni 15 ili kukamilish a ujenzi huo ikiwa pia ni kwa Heshma ya Baba wa Taifa Mwalim Julius Kambarage Nyerere ambae ndie alieanza Kuijenga Hospitali hiyo.