Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere - Mara

WAUGUZI MARA WAKUMBUSHWA KUZINGATIA MAADILI YA KAZI

Posted on: May 12th, 2020

Muuguzi mkuu wa Mkoa wa Mara Ndg,Stanley Kajuna amewataka wauguzi  kuzingatia maadili,kanuni na taratibu za kazi ili kulinda taaluma zao na kuhakikisha wanatoa huduma bora kwa jamii. Kauli hiyo ameitoa leo ikiwa ni maadhimisho ya  miaka 200 ya siku ya wauguzi duniani ambayo hufanyika Mei 12 kila mwaka ikiwa ni sehemu ya kumuenzi Muasisi  wa taaluma ya kiuguzi duniani  bi. Frolence Nightngale ambaye alitumia muda wake mwingi kuhudumia wagonjwa kwa moyo wa huruma,upendo na Amani.

Bwn,Kajuna amesema, njia pekee ya kumuenzi Muasisi wa taaluma ya Uuguzi ni wauguzi kuendelea kuwapenda na kuwahudumia wagonjwa wote kwa upendo,usawa na ukaribu katika mazingira yaliyopo na kuhakikisha wanapata huduma nzuri.

Ameendelea kusema kuwa ,kutokana na janga la mlipuko wa ugonjwa wa corona (covid-19) mwaka huu sherehe hizi zitaadhimishwa tofauti kwa kutokuwa na mkusanyiko wowote ila kazi za kuhudumia wagonjwa zinaendelea kufanyika.

Amesema “Natambua  mchango wa wauguzi katika kuimarisha afya ya jamii ni mkubwa na hauna kipimo hasa katika kipindi hiki ambapo mpo msitari wa mbele kapambana na janga hili la corona,hivyo nawatia moyo na muendelee kusaidia wananchi pasipo kukata tamaa”

Kwa upande wake mwenyekiti wa TANNA (Tanzania National Nursing Association) Mkoa wa Mara Ndg,Ngeleja Lupeleleja ambaye pia ni Muuguzi katika Hospitali ya Rufaa  Mkoa wa Mara amewapongeza wauguzi kwa kuendelea kuwa na moyo wa  huruma na kujitolea,kwa kutumia muda wao mwingi kutoa huduma zilizo bora kwa jamii pasipo kujali changamoto zilizopo.

Bw. Ngeleja amesema kuwa, wauguzi wamekuwa msitari wa mbele kuhakikisha jamii inakuwa na afya bora kwa kutoa elimu,ushauri na kuwahudumia wagonjwa kwa moyo wa dhati,Hivyo anatoa wito kwa serikali  kusaidia kutatua changamoto zinazowakabili wauguzi kama kuwapatia motisha na stahiki zao ikiwemo  kupandishwa madaraja kwa wakati,kupatiwa vifaa tiba na kinga, kupunguza ongezeko la ada ya leseni pamoja na kupewa posho za sare na kazi za ziada

Pia amesema Mkoa wa mara unakabiliwa na upungufu wa wauguzi kwa asilimia 49,hivyo ni ombi lake kwa kwa serikali ya Awamu ya Tano  ya Mh.Rais John Pombe Magufuli kuangalia namna ambayo wanaweza kusaidia kuongeza wauguzi ili kazi ya kutoa huduma kwa wananchi iendelee kuwa bora Zaidi.

Kwa upande wake katibu wa TANNA  Mkoa wa Mara Onkwani Lazalous pamoja na wauguzi wanasema wanajivunia mafanikio wanayoyapata katika chama cha wauguzi  ikiwemo kuweza kuwaunganisha na kuwaleta pamoja wauguzi wote, kusikiliza changamoto zao na  kuzitatua.Hivyo wanaendelea kuiomba serikali kushirikiana nao kwa ukaribu  katika kuzitatua changamoto zao na  kuboresha mazingira ya utendaji kazi ili kuwalinda wauguzi na kuwafanikisha kutoa huduma bora kwa jamii.

Sambamba na hilo wauguzi wametakiwa kuhudumia jamii  kwa moyo wa kujitolea kulingana na Kauli mbiu ya maadhimisho ya sikukuu ya wauguzi duniani mwaka huu ambayo ni “Wauguzi,sauti inayoongoza Uuguzi kwa Dunia yenye  Afya”.