Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere - Mara

WAUGUZI MARA :TOENI HUDUMA BORA KWA WANANCHI

Posted on: May 21st, 2021

Watumishi Wauguzi Mkoa wa Mara wanakumbushwa kumuenzi muasisi taaluma ya Uuguzi Bi.Frorence NightNgale kwa  kuendelea kufanya kazi kwa bidii,weledi na kujituma huku wakizingatia maadili miongozo na miiko ya kazi yao pindi wanapotoa huduma kwa wagonjwa.


Kauli hiyo imetolewa na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mara Dkt.Frolian Tinuga kwa Niaba ya Katibu Tawala Mkoa Bi Carolina Mthapula wakati wa Maadhimisho ya Kimkoa ya sherehe  ya siku ya  wauguzi Duniani inayofanyika tarehe 12 Mei kila mwaka na Kimkoa  imefanyika leo katika Halmashauri ya Wilaya ya Bunda.


''Serikali na Mkoa unatambua na kuthamini mchango na kazi kubwa na ngumu inayofanywa na wauguzi katika kutoa huduma kwa jamii,na mahali popote ukisikia Hospitali fulani inafanya vizuri Basi ujue ni wauguzi wanafanya vizuri maana wao ndio wanawapokea wagonjwa,wanakuwa nao na kutumia muda wao mwingi kuhudumia''. 


Amesema,wauguzi ni watu muhimu Sana katika idara ya Afya maana wanawasaidia wagonjwa katika mazingira yote  pasipo kujali utaalamu wa mtu mwingine hususani pale wanaposaidia  binadamu kuwepo Duniani na pindi wanapoondoka Duniani hivyo Uuguzi ni kazi ya wito isiyo na malipo yeyote zaidi kuwa na moyo wa upendo na huruma.


Aidha Dkt.Tinuga amewaasa wauguzi kuacha kufanya vitendo vilivyo kinyume na maadili yao ikiwemo matumizi ya lugha Kali zisizo na uvumilivu kwa wateja,kutotoa taarifa sahihi na kwa wakati kwa wateja,kupenda kuwa wasemaji wa taasisi na kupokea pesa kutoka kwa wateja Kwani vitendo hivi vinasababisha kuwepo na malalamiko mengi yanayopelekea kuichafua taaluma ya uuguzi.


Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Bunda Mhe.Lydia Lupilipi amewataka wauguzi kuendelea kushikamana na kujali Afya za wananchi na pale wanapoona changamoto zinazidi Basi wavumilie na kusubiri kutatuliwa.

" Kazi zote zina changamoto lakini pamoja na hayo inabidi watumishi tujitunze,tujikubali, tuvumilie,tuipende na kufanya kazi yetu kwa Moyo".

Aidha ametoa wito kwa viongozi na wakuu wa idara kutotumia madaraka yao vibaya kutojali maslahi ya wauguzi badala yake watatue changamoto zinazowakabili ikiwemo watumishi kupatiwa motisha na kushughulikia maombi yao na kuyatolea ufafanuzi..


Maadhimisho haya yameenda sambamba na Kutoa huduma za ushauri nasaha na kupima VVU,Ushauri wa Afya ya mama na mtoto, wauguzi kutembelea wagonjwa na Kutoa msaada katika Hospitali ya kibara,kurudia kuapa kiapo chao Cha kazi pamoja na  kupewa vyeti na zawadi kwa kutambuliwa kuwa na mchango mkubwa  katika majukumu ya kazi.