Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere - Mara

WATUMISHI WATAKIWA KUZINGATIA MAADILI N NIDHAMU KAZINI

Posted on: July 31st, 2021


Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara Dkt.Joachim Eyembe amewataka watumishi wa sekta ya Afya kufanya kazi kwa kuzingatia madili, nidhamu na taratibu za kiutumishi katika kutekeleza majukumu ya kila siku.

Dkt. Eyembe ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na watumishi pamoja na wadau wa sekta ya afya Mkoa wa Mara katika Hafla ya kumpongeza na kumuaga aliyekua Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mara Dkt.Florian B.Tinuga katika ukumbi wa Dream Garden uliopo katika Manispaa ya Musoma.

“Niwaombe tulikumbuke suala la nidhamu kwa sababu ndio msingi mkubwa unaotuwezesha kutekeleza majukumu yetu kiufanisi ndani ya utumishi wa umma”alisema Eyembe

Amesema nidhamu ni kutekeleza majukumu yako binafsi pamoja na unayopangiwa na kiongozi wako kwa ufanisi na wakati ili iweze kuleta tija katika nafasi unayoitumikia na si kufanya kinyume ya hapo.

Aidha dkt.Eyembe amewataka watumishi kudumisha upendo,umoja,heshima na ushirikiano katika kutekeleza majukumu yao na kuziondoa tofauti na  changamoto baina ya mtu na mtu kwani zinazorotesha ufanisi wa kazi.

“Fanyeni kazi kwa umoja na ushirikiano huku mkisaidiana kwani mafanikio yeyote hutokea si kwa mtu binafsi bali kwa kutegemeana katika kutekeleza majukumu”alisema Eyembe

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mara Dkt.Florian B. Tinuga amewashukuru watumishi wote wa Mkoa wa Mara kwa Ushirikiano waliompatia pamoja na matokeo mazuri yaliyopatikana wakati akitekeleza majukumu yake katika Mkoa huo.

“Niwashukuru na kuwapongeza watumishi wenzangu kwa ushirikiano mlionipatia hususani katika suala la kuwa na nidhamu maana mlitekeleza ipasavyo majukumu tuliyopangiana yakaleta matokeo mazuri na hiyo ndio nidhamu ninayotaka muendelee kuwa nayo hata kwa kiongozi mwingine atakayekuja”alisema Tinuga

Aidha amesisitiza suala la uwajibikaji na kuendeleza ushirikiano wa pamoja kuanzia ngazi ya Mkoa,RHMT,CHMT pamoja na watumishi wengine katika kutekeleza majukumu ikiwa ni pamoja na kujengeana uwezo na kufundishana kwani kwa kufanya hivyo kutaleta mafanikio chanya katika maendeleo ya sekta ya afya ndani ya Mkoa.

Aidha amewaomba watumishi kumpatia ushirikiano RMO atakayekuja kwa kuendelea kusimamia matokeo yaliyopatikana wakati wa utumishi wake ikiwemo kupunguza Vifo vya Mama na Mtoto pamoja na kupunguza Maambukizi ya Malaria ndani ya Mkoa ili wananchi Wanufaike na huduma bora za afya tunazozitoa.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na timu ya usimamizi wa huduma ya afya ngazi ya Mkoa na Halmashauri{RHMT &CHMT’S},Watumishi wa ofisi ya Katibu Tawala Mkoa-RS,Wadau wa Afya wanaotekeleza majukumu yao katika Mkoa wa Mara pamoja na Watumishi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara.