Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere - Mara

WANANCHI MARA WATAKIWA KUCHUKUA TAHADHARI DHIDI YA CORONA

Posted on: April 16th, 2020

Wananchi wa Mkoa wa Mara wameshauriwa kuchukua tahadhari ili kujikinga na maambukizi ya virusi vya ugonjwa wa  Corona (COVID -19).Ushauri huo umetolewa Leo na Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Adam Kighoma Malima kwenye uzinduzi wa zoezi la kupulizia dawa  magari ya abiria yanayofanya safari zake maeneo mbalimbali ndani na nje ya Mkoa wa Mara lengo ikiwa ni kuhakikisha usalama wa abiria muda wote wakiwa ndani ya magari ,zoezi ambalo limefanyika katika stendi kuu ya mabasi  iliyopo eneo la Bweri katika manispaa ya Musoma.

Akizungumza katika zoezi hilo, amesema kuwa kuanzia sasa hakuna gari yeyote itakayotoka kituoni bila kupulizwa dawa hivyo  wamiliki wote wa magari na madereva wahakikishe magari yao yanapigwa dawa  nusu saa kabla ya kuanza safari huku akiwataka kuweka  maji yenye dawa pamoja na vitakasa mikono ndani ya gari kwa ajili ya abiria kutumia wakiwa safarini na atakayekiuka agizo hilo hatua kali za kisheria zitachukuliwa.

Aidha Mhe.Malima amewataka wakazi wote wa Mkoa wa Mara kuchukua tahadhari ikiwemo kunawa mikono kwa sabuni na maji tiririka kila wakati,kuacha tabia ya kusalimiana kwa kushikana mikono na kukumbatiana, kufunika mdomo pindi wanapokohoa au kupiga chafya pamoja na kuepuka misongamano na safari zisizokuwa za lazima.

‘’Amesema kuwa hadi sasa hakuna mtu aliyethibitika kuwa na ugonjwa hapa kwetu ila ugonjwa upo kwa kiwango kikubwa hivyo ni lazima tuchukue tahadhari na kufuata  maelekezo tunayopewa  na wataalamu wetu wa afya pamoja na viongozi wa serikali’’.

Sambamba na hilo Mhe.Malima amemuagiza Mkurugenzi wa  mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira Musoma (MUWASA) CPA.Joyce Msiru kuboresha miundombinu ya maji na kuhakikisha maji yanapatikana muda wote stendi kuu ya mabasi Bweri ili watumiaji wa stendi hiyo waweze kunawa mikono mara kwa mara ikiwa ni namna ya kujikinga na maambukizi. 

Agizo hilo amelitoa baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa watumiaji wa stendi hiyo juu ya ukosefu wa maji mahali hapo jambo ambalo linakwamisha  utekelezaji wa agizo la serikali kunawa mikono kwa maji tiririka.

‘’Amesema kuwa serikali hatuwezi kuwaambia wananchi wanawe mikono wakati hakuna maji ya kutosha,hivyo nahitaji maji yapatikane muda wote wananchi waweze kunawa mikono’’.

Kwa upande wao wananchi wameishukuru serikali kwa juhudi na hatua wanazochukua kupambana na ugonjwa huu wa Corona ikiwemo kuendelea kutoa elimu kwa wananchi namna ya kujikinga na maambukizi ya virusi vya COVID-19.