Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere - Mara

SIMAMIENI MIIKO YA KAZI ZENU ILI MTOE HUDUMA BORA KWA WANANCHI

Posted on: August 5th, 2024

Watumishi wa afya mkoani Mara wameaswa kutoa huduma bora kwa weledi na kuzingatia maadili ili kuendelea kutoa huduma bora kwa wananchi wanao fika Hospitali hapo kupata huduma za kimatibabu.

Hayo yamesemwa Agosti 05, 2024 na Mkuu wa mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi wakati akiongea na watumishi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa huo ya Mwalimu Nyerere mara baada ya kufanya ziara ya kuangalia hali ya utoaji huduma na maendeleo ya ujenzi wa Hospitali.

Kanali Evans Alfred Mtambi amesema kuwa Hospitali ya Rufaa iwe ni kituo chakurudisha uhai na matumaini kwa wananchi hivyo akahimiza weledi na kuzingatia maadili ili kuokoa afya za wananchi.

“Tunahitaji Hospitali hii ya Rufaa iwe ni kituo ambacho kitamrudishia mwananchi matumani ya afya yake baada ya kufika kwa matibabu",amesema Kanali Evans Alfred Mtambi

Aidha, Kanali Mtambi amewapongeza watumishi wanaojitoa kuhudumia wananchi na ameongezea kuwa serikali itaendelea kuzifanyia kazi changamoto kadha zinazojitokeza za watumishi huku akiwataka kuendelea kutimiza wajibu wao wa kuhudumia wananchi.

Akiwasilisha taarifa ya Hospitali Mganga Mfawidhi wa Hospitali Dkt. Osimund Dyegura amesema kwasasa kuna changamoto ya rasilimali watu ambayo haikidhi mahitaji ambayo ni makubwa kwa wagonjwa wanaofika kupata huduma.

Pia, Dkt Osimund ameongezea kuwa katika kukabiliana na changamoto ya rasilimali watu Hospitali inatarajia kupokea ajira mpya na imeajiri watumishi wa mkataba 81.

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mara Dkt. Zabron Masatu ameishukuru Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara kwa kazi kubwa inayofanyika kuhakikisha miundombinu ya Hospitali inakamilika.

Pia, Dkt Masatu amemuhakikishia Mkuu wa Mkoa kuwa huduma katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere zitaendelea kutolewa kwa kufuata maadili, kanuni na taratibu zilizo wekwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Wizara ya Afya.