Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere - Mara

QIT-KUTUMIA RASILIMALI ZILIZOPO KUTATUA CHANGAMOTO ZA UTOAJI HUDUMA

Posted on: September 18th, 2020

Timu ya Maboresho ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara (Quality Improvement Team) wameshauriwa kutumia weledi na rasilimali walizonazo ili kutatua changamoto zilizopo  na kuhakikisha wanatoa huduma bora kwa wananchi.

Ushauri huo umetolewa  na Muuguzi Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara Bwn.Joachim Masunga kwa niaba ya Mganga Mfawidhi wakati akiahirisha kikao cha siku tatu cha kujengeana uwezo (competence check)baina ya wajumbe wa timu ya maboresho ya hospitali pamoja na wawezeshaji kutoka Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto kitengo cha maboresho na huduma bora kilichofanyika katika ukumbi wa jengo la grade uliopo katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara.

Akizungumza katika kikao hicho Bwn. Masunga amesema kuwa,lengo la mafunzo hayo ni kujengeana uwezo ili kuweza kusimamia utoaji bora wa huduma kwa kuzingatia viwango vilivyowekwa  hivyo ili kuboresha huduma kwa wateja mafunzo na elimu  iliyotolewa ikatumike vyema katika uhalisia na kwa kushirikishana  ili dhana nzima ya maboresho ikatekelezeke na kuonekana.

“Mafunzo mliyoyapata mkayafanye katika uhalisia kwa kushirikiana na watumishi wengine ili huduma ziweze kuboreka na kutolewa vizuri kulingana na miongozo ya taasisi na serikali yetu.”

Aidha ameongeza kusema kuwa kufanya kazi kwa umoja na ushirikiano kutaongeza ufanisi ambao utasababisha kuimarika kwa huduma  na  kupunguza vikwazo kwa wateja wetu jambo ambalo ni muhimu sana katika utoaji  wa huduma bora kwa wananchi na maendeleo ya taasisi.

Kwa upande wao Wawezeshaji wa Mafunzo haya wameshukuru kwa ushirikiano walioupata kutoka kwa uongozi pamoja na wajumbe wa timu ya maboresho na kusema kuwa umoja na ushirikiano uliopo uendelee kuwepo pia katika kazi na ili mafunzo haya yawe na faida basi ni jukumu la timu ya maboresho kuyatoa kwa watumishi wengine  na kufanyia kazi kama yalivyofundishwa.