Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere - Mara

MWENYEKITI UVCCM TAIFA APONGEZA UJENZI WA HOSPITALI YA MWL.NYERERE

Posted on: July 1st, 2020


 

Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa chama cha Mapinduzi  CCM Taifa ,Comrade Herry James ameipongeza serikali ya awamu ya tano kwa   kumuenzi na kutimiza kwa vitendo ndoto ya  Baba wa Taifa Mwl.Julius Nyerere ya kuleta huduma ya afya kwa wananchi wa Mkoa wa Mara.

Comrade Herry amesema hayo leo alipotembelea na kukagua mradi wa ujenzi wa hospitali ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere – Kwangwa iliyopo Manispaa ya Musoma Mkoani Mara.

Amesema”kuendelea kuwa na fikra za kumuenzi Baba wa Taifa kwa vitendo kutailinda heshima yake na kubeba historia ya nchi yetu.’’

Aidha amempongeza Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe.Adam  Malima pamoja na Uongozi wa hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara kwa kusimamia na kuhakikisha ujenzi wa hospitali hiyo unafanyika kama ilivyopangwa na kusema Mkoa wa Mara ni mfano wa Mikoa ambayo wazawa wake wanafanya kazi kubwa ya kutekeleza miradi ya maendeleo kwa nguvu zao.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe.Adam Malima amesema anatarajia ifikapo julai 30 jengo la mama na mtoto katika hospitali hiyo litafunguliwa na wananchi kuanza kupata huduma kwa sababu tayari wamepokea fedha takribani billioni nne(4) kwa ajili ya kumalizia ujenzi huo na tayari ameshaanza kupokea ahadi za vitanda na magodoro kutoka kwa wadau mbalimbali.

Awali akimpokea Mwenyekiti wa UVCCM Taifa, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara Dr.Joachim Eyemba ameeleza  kuwa changamoto za kiutendaji zilizokwamisha ujenzi huu  zimetatuliwa na kwa sasa timu yote ya Mkoa pamoja na mshauri mwelekezi wa mradi wapo site,hivyo ametoa maelekezo kuwa kazi zifanyike usiku na mchana ili kuhakikisha mradi huu unakabidhiwa kwa wakati.

Sambamba na hilo Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) ambalo ndio wakandarasi wa mradi huu wamepewa pongezi kwa kazi kubwa wanayoifanya na kuhimizwa kuikamilisha kwa wakati ili wananchi waanze kupata huduma.