Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere - Mara

MSHAURI MWELEKEZI AKWAMISHA UJENZI HOSPITALI YA MWL.NYERERE

Posted on: June 8th, 2020

MSHAURI MWELEKEZI AKWAMISHA UJENZI HOSPITALI YA MWL.NYERERE 

 

Ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere - Kwangwa uliokuwa mbioni kukamilika chini ya Mkandarasi  Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), umekwama kwa zaidi ya mwezi mmoja baada ya Mshauri Mwelekezi wa Mradi huo ambae ni Chuo cha Ardhi kusimamisha ujenzi huo pasipo kutoa sababu za msingi.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kukagua Jengo hilo Leo, Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mh.Angeline Mabula ameshangazwa na hatua iliyochukuliwa na mshauri mwelekezi wa  kusimamisha  ujenzi wa mradi huo pasipo idhini ya Mwajiri ambae ni Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii Jinsia na Watoto Kwani ndiye mwenye mamlaka ya kufanya hivyo.

Mh.Mabula amesema kuwa amesikitishwa sana na kitendo cha kusimama kwa mradi huo uliogharimu kiasi kikubwa cha fedha kwa sababu kazi inayosimamishwa asilimia sabini (70%)Shirika la nyumba la taifa imeshafanya, na kwa kufuata maelekezo ya mshauri huyo tayari wameshanunua vifaa vyote vya kukamilisha ujenzi huo  kwa kutumia fedha zake za ndani.

“Haiwezekani mshauri kusimamisha kazi akiwa nje ya site pasipo kujua kazi inaendaje,hivyo katika kukagua naona kuna uwalakini katika utendaji kazi wa mshauri huyu.”

Kutokanana hali hiyo Mh.Mabula amewatoa hofu wananchi na kuahidi, serikali kupitia Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto pamoja na Wizara ya Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi watachukua hatua za haraka kutatua changamoto hii ikiwa ni pamoja na kubaini sababu zilizopelekea mshauri kusimamisha mradi huu wa kimkakati  pamoja  na kujua hatma yake.

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Musoma Mjini Mh.Vedastus Mathayo amesema kuwa amesikitishwa na kitendo hiki na kuahidi kuwa atalifuatilia kwa ukaribu suala hili ili wanachi  wa Mkoa wa Mara waweze kupata huduma za Afya katika Hospitali hii kabla ya mwisho wa mwaka huu kama ambavyo waliahidiwa maana vifaa vyote vya kukamilisha ujenzi vipo.

Nae katibu wa Afya wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara Bi Masuda Gasper amesema kuwa wao kama taasisi ya afya wameathika kutokana na kitendo hiki sababu mategemeo yao ilikuwa hospitali iishe kwa wakati hivyo,amezishauri mamlaka husika zifuatilie jambo hili ili hospitali iweze kukamilika kwa wakati kama ilivyopanga na wananchi waweze kupata huduma muhimu.

Sambamba na hilo Mh.Mabula amelipongeza shirika la nyumba la Taifa (NHC) kwa  uzalendo na juhudi wanazozifanya katika kuhakikisha ujenzi wa mradi huu unakamilika kwa wakati kiwemo kutumia fedha zao za ndani ili ujenzi usisimame.