Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere - Mara

MAFUNZO YA 5'S-KAIZEN KUSAIDIA KUBORESHA UTOAJI WA HUDUMA

Posted on: February 24th, 2021

Timu ya Udhibiti Ubora Wa Huduma ya  Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara(QUALITY IMPROVEMENT TEAM-QIT) Leo imeendesha mafunzo ya siku moja ya 5’S-Kaizen kwa Watumishi wa kitengo cha dharula cha hospitali lengo ikiwa ni kujengeana uwezo wa nanma  ya kuboresha utoaji wa huduma bora kwa wagonjwa kwa kuangalia mapungufu yaliyopo sasa na kuyawekea mkakati wa kukabiliana nayo.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo Mwenyekiti wa kitengo cha udhibiti Ubora katika hospitali  ya Rufaa ya Mkoa wa Mara ndg.Venance Bwire amesema kuwa mafunzo haya yanalenga kukumbushana na kujengeana uwezo wa namna bora ya utekelezaji wa majukumu hususani kutathmini njia bora ya kufanya ili kuboresha utoaji wa huduma ikizingatiwa kitengo cha dharula ni kitengo kinachoona wagonjwa wenye kuhitaji msaada na huduma ya haraka ili kuokoa maisha yao.

Amesema kuwa,iwapo kitengo cha dharula kitaboreshwa na watumishi wake kujengewa uwezo wa utoaji huduma ipasavyo kwa kuzingatia taratibu na maadili ya utumishi wa umma ikiwemo kutumia nyenzo ya  5’S –KAIZEN kama muongozo katika utekelezaji wa majukumu yao ya utoaji wa huduma basi kitasaidia kwa kiasi kikubwa kuleta matokeo chanya ya utoaji wa huduma katika hospitali.

“Kitengo cha dharula kikiboreshwa vyema itasaidia kuongeza ufanisi katika kazi ,kuongeza mapato ya hospital pamoja na kusaidia kutoa huduma bora itakayopelekea  wateja kuridhika na kupunguza malalamiko yanayosababisha kuharibu taswira ya Hospitali.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa kamati ya 5’S-KAIZEN katika kitengo cha Udhibiti Ubora Bi.Magreth Abel amewataka watumishi wa kitengo cha dharula kujenga mshikamano na ushirikiano katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku huku akisisitiza  kuhusu uwajibikaji na umiliki binafsi wa majukumu pasipo kutengeana na kuona jukumu Fulani linastahili kufanywa na mtu Fulani.

‘’Amesema ili huduma ziboreke ni muhimu kila mmoja kuacha tabia ya kufanya kazi kwa mazoea badala yake  wajitume na kuwa na umoja utakaoleta tija katika maendeleo ya kitengo na taasisi ikiwemo kuongezeka kwa morali ya kazi kwa watumishi na kuongezeka kwa  mapato.

Aidha kwa Upande wao watumishi wa kitengo cha Dharula wameshukuru kwa mafunzo waliyopata na kuahidi kuyatumia ipasavyo katika kuboresha utoaji wa huduma  kwa wagonjwa huku wakisisitiza kufanya kazi kwa weledi na ushirikiano kila mmoja katika nafasi yake.