KLINIKI TEMBEZI KUTUMIKA KUIBUA WAGONJWA WA TB, UKIMWI NA MALARIA
Posted on: November 9th, 2023KLINIKI TEMBEZI KUTUMIKA KUIBUA WAGONJWA WA TB, UKIMWI NA MALARIA
Na. WAF - Dodoma
Waziri wa Afya Mhe. @ummymwalimu amesema magari ya Kliniki Tembezi (Mobile Clinic) yakatumike katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Kifua Kikuu (TB) hususani kuibua wagonjwa wapya, UKIMWI, Malaria pamoja na Magonjwa Yasiyoambukiza ikiwemo Kisukari.
Waziri Ummy amesema hayo Novemba 8, 2023 wakati wa makabidhiano ya magari hayo ya Kliniki Tembezi yenye thamani ya Mil. 618,477,000/= yaliyofanyika Mkoani Dodoma.
“Karibu 35% ya wagonjwa wa Kifua Kikuu bado tunao katika majumba yetu, ofisi zetu, vijiji vyetu na mitaani kwetu, Kwahiyo naamini kabisa magari haya yatatumika katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa TB kwa kuibua wagonjwa wapya, mapambano dhidi ya Malaria na UKIMWI”. Amesema Waziri Ummy
Aidha, Waziri Ummy amesema magari hayo (Mobile Clinic) yatakuwa yanatoa huduma za Afya za kisasa katika jamii ambayo ipo mbali na huduma za Afya pamoja na kutembea katika masoko na stendi za magari kutoa huduma za upimaji.
Aidha Waziri Ummy amesema, Tanzania ina changamoto ya magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo Kisukari ambapo katika kila watu 100 wenye umri wa miaka 15 na kuendelea watu 9 wana ugonjwa wa Kisukari, changamoto ya watu wenye Shinikizo la Juu la Damu ambao ni 25% na hawajui.
“Nitoa shukrani nyingi sana kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kujali Afya za Watanzania kwa kuendeleza mashirikiano na Mataifa mbalimbali na kuja kuwekeza nchini hasa katika Sekta ya Afya”. Amesema Waziri Ummy
Mwisho, Waziri Ummy ameshukuru uongozi wa Aga Khan - Tanzania na Benki ya Maendeleo ya Ujerumani (KFW) kwa kuwekeza kwenye Sekta ya Afya na kwa kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali ya Rais Samia katika kuboresha mifumo ya utoaji wa huduma za Afya nchini.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu OR - TAMISEMI Dkt. Wilson Mahera amesema magari hayo (Kliniki Tembezi) yatakwenda kusaidia upatikanaji wa huduma za Afya kwa haraka katika Jamii ambazo zipo mbali na vituo vya Afya.