Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere - Mara

HUDUMA ZA KIBINGWA ZATOLEWA MARA

Posted on: October 7th, 2021

Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara kwa kushirikiana na Hospitali ya Kanda Bugando  inaendesha zoezi la kutoa huduma za kibingwa kwa wananchi wa Mkoa wa Mara na maeneo Jirani ikiwa ni sehemu ya kuelekea kilele cha maadhimisho ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwa huduma katika hospitali ya kanda Bugando.

Akizungumza wakati wa zoezi hilo Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara na daktari bingwa wa Mifupa Dr. Elius Godfrey ameishukuru Hospitali ya Kanda ya Bugando kama walezi wa hospitali za Mikoa za kanda ya ziwa kuona umuhimu wa kutoa madaktari bingwa kwa ajili ya kwenda  kutoa huduma za kibingwa kwa wananchi wa Mkoa wa Mara.

“Hospitali imeweza kupokea madaktari bingwa sita{6}kutoka katika fani mbalimbali ikiwemo  magonjwa ya mfumo wa mkojo,Upasuaji wa jumla {general surgery}, magonjwa ya Koo,Pua na Masikio,magonjwa ya ndani,afya ya akili na upasuaji sanifu{plastic surgery} ,amesema Dr.Godfrey.”

Aidha amesema zoezi la utoaji wa huduma limefanikiwa kwa kiasi kikubwa ambapo kwa siku wameweza kuhudumia  wagonjwa mia mbili {200) na   kufanya pasuaji 13 na idadi inatarajiwa kuongezeka kutokana na huduma hizi kuendelea  kutolewa kwa muda wa siku tatu.

Sambamba na hilo Dr. Elias ameainisha huduma za kibingwa zinazotolewa katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara ikiwemo huduma mpya ya uchunguzi wa afya ya Moyo {Echocardiograpy} ambayo imeanza kutolewa kwa mara ya kwanza katika Mkoa wa Mara,huduma za usafishaji figo {dialisisy},huduma za mifupa Pamoja na huduma za magonjwa ya akina mama.

Aidha ameishukuru Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto kwa kutoa kipimo hicho  cha Uchunguzi wa Moyo kwa sababu  kitasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza gharama kwa wananchi kusafiri na kufuata huduma hiyo muhimu katika hospitali ya Kanda Bugando ama maeneo mengine.

Kwa upande wake daktari bingwa wa Upasuaji wa Koo,Pua na Masikio {ENT} Kutoka Hospitali ya Kanda Bugando Dr.Gustave Buname amesema kuwa, katika kuadhimisha miaka 50 tangu kuanzishwa kwa hospitali ya Kanda Bugando,Taasisi imeamua kutoa madaktari bingwa  kuzungukia Mikoa yote ya kanda ya ziwa ili kutoa huduma kwa wananchi kwenye hospitali za Mikoa,Wilaya na Mashirika ya dini kama sehemu ya shukrani kwa wananchi na wadau wote wanaoshirikiana kuunga mkono jitihada za taasisi hiyo katika kuboresha huduma na kupata mafanikio.

“Tumeamua kufanya huduma hii kama sehemu ya kurudisha shukrani kwa wananchi na wadau wanaotuunga mkono kuhakikisha taasisi yetu imepata mabadiliko makubwa hususani katika utoaji wa huduma ukilinganisha na kipindi cha nyuma ambapo kwa sasa tumeongeza uwigo wa idadi ya wagonjwa tunaoweza kuwahudumia kwa wiki ni takribani 6500 na pasuaji 70 kwa siku na huduma zimeweza kuboreshwa katika nyaja zote za rasilimali watu,vifaa tiba na madawa pamoja na kuwa na taasisi za elimu hivyo kwetu haya ni mafanikio makubwa hatuna budi kujivunia”.

Aidha amebainisha changamoto kubwa wanayokutana nayo katika maeneo mengi kuwa ni Pamoja na wagonjwa wengi kufika kupata huduma wakiwa wamechelewa sana na kusababisha utatuzi wa matatizo yao kutowezekana kufanyika katika maeneo yao hivyo ametoa rai kwa wananchi kujenga mazoea ya kufanya uchunguzi wa afya zao mapema na kupata matibabu pasipo kusubiri mpaka waugue.

Kwa upande wao wananchi wameshukuru kwa huduma walizozipata na kuomba huduma kama hizi zifanyike mara kwa mara ili kuwasaidia wananchi ambao wanauhitaji na hawana uwezo wa kuzifuata maeneo ya mbali huku wakiipongeza serikali kwa kuona umuhimu wa kuzipa kipaumbele na kuziboresha  hospitali za Rufa za Mikoa katika kutoa huduma kwa wananchi.