Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere - Mara

HUDUMA ZA KIBINGWA KUTOLEWA HOSPITALI TEULE YA WILAYA YA SERENGETI-NYERERE DDH

Posted on: February 21st, 2021

Mganga Mfawidhi wa Hospitali Teule ya Wilaya ya Serengeti-Nyerere DDH Dkt. Tanu Warioba, amewataka wananchi wa Wilaya ya Serengeti pamoja na maeneo jirani kutumia fursa ya ujio wa Madaktari Bingwa kama Neema kwao itakayowafanya waweze kupata huduma mbalimbali za kibingwa ndani ya Wilaya yao kwa urahisi na gharama nafuu pasipo kufuata huduma hizo katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa.

Dkt.Tanu amesema hayo leo wakati wa kuanza kwa zoezi la siku saba la utoaji wa huduma za Kibingwa za  Mkoba zinazotolewa hospitalini hapo  na  Madaktari Bingwa kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara ambapo Huduma zitakazotolewa ni pamoja na huduma za upasuaji wa kawaida, mifupa,koo na masikio,huduma za matibabu ya akina mama na watoto,matibabu ya njia ya mkojo pamoja na huduma za matibabu ya magonjwa ya ndani.

Amesema kuwa, kumekuwa na changamoto ya upatikanaji wa huduma za kibingwa katika hospitali hiyo Teule ya Wilaya  jambo linalosababisha kuwepo kwa Rufaa nyingi kwa wagonjwa kufuata huduma katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa-Musoma ama katika Hospitali zingine nje ya Mkoa,Hivyo ujio wa Madaktari  katika hospitali hiyo kutasaidia wananchi kwa kiasi kikubwa kupata huduma za kibingwa pamoja na matibabu.

Nae daktari Bingwa wa Mifupa kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara Dr.Elius Godfrey amesema kuwa lengo la kufanya huduma hii ya Mkoba ni   kusogeza huduma za kibingwa karibu na wananchi pamoja na kupunguza gharama za matibabu na usafiri ambazo wananchi wanalazimika kutumia kufuata huduma hizo katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa.

Amesema kuwa, kutoa huduma hizi Leo katika Hospital ya Nyerere DDH ni mwendelezo wa utaratibu wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara kutembelea na kufanya huduma ya   Mkoba kila robo ya mwaka kwa hospitali wanazozisimamia ndani ya Mkoa

Kwa upande wao wananchi wa Wilaya ya Serengeti wameushukuru uongozi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara pamoja na Hospitali Teule ya Wilaya ya Serengeti kuona umuhimu wa kufanikisha  ujio wa Madaktari bingwa katika hospitali yao  kwani kwa kiasi kikubwa itasaidia kutatua changamoto za upatikanaji wa huduma hizo za kibingwa  wanazozikosa na pia itaokoa gharama kubwa wanazolazimika kutumia kufuata huduma  katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa ama Hospitali ya kanda Bugando.

Vilevile wananchi wametoa wito kwa Hospital ya Rufaa ya Mkoa wa Mara kuendelea kutoa huduma muhimu ili kusaidia  wananchi  hususani waliopo maeneo ya wilayani ambapo huduma hizi hazipatikani kwa wakati na pia wanatoa ombi kwa Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto kuendelea kuboresha huduma za Afya  hususani kuongea Madaktari bingwa watakaoweza kuhudumia na kuwafikia wananchi katika ngazi za Hospitali za Wilaya.