Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere - Mara

HUDUMA YA UPASUAJI WA MIFUPA IMEANZA RASMI KATIKA HOSPITALI YA MKOA WA MARA

Posted on: January 5th, 2020

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara Dr Joachim Eyembe, Leo amekabidhi vifaa vya upasuaji wa mifupa kwa Daktari bingwa wa mifupa Dr Elias Godfrey vyenye thamani ya Shilingi milioni 40 ikiwa ni sehemu ya vifaa vinavyohitajika ambavyo vinakadiriwa kufikia gharama ya jumla ya shilingi milioni 200, ambavyo vimenuniliwa kwa fedha za makusanyo ya Hospitali.

Akikabidhi vifaa hivyo Dr Eyembe amesema kuwa upasuaji wa mifupa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara umeanza rasmi leo hivyo anawakaribisha wananchi wa Musoma hususani Mkoa wa  Mara  kufika na kupata huduma hii badala ya kuzifuata katika vituo vingine vya afya au hospital kubwa zilizopo nje ya mkoa wa mara.

Aidha ameongeza kuwa hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara imekuwa miongoni mwa Hospitali za Rufaa za mikoa za  mwanzo kupata daktari bigwa wa mifupa,lakini pia kuwa na uwezo wa kuwa na vifaa vya kumuwezesha daktari huyo kuweza kufanya kazi kwa ufanisi.

Kwa upande wake  daktari bingwa wa mifupa ameshukuru uongozi wa hospitali ya rufaa ya Mkoa wa mara chini ya mganga mfawidhi Dr. Eyembe kwa vifaa vya upasuaji wa mifupa ambavyo wamepatiwa na kuahidi kuwa yeye pamoja na timu yake wamejipanga vyema kuanza kutoa huduma rasmi. Dr Elias ameongeza kuwa huduma ya upasuaji itakuwa inatolewa siku ya Jumanne na Alhamis lakini kwa huduma za dharula huduma itapatikana kila siku.

Katika makabidhiano hayo baadhi ya vifaa vilivyonunuliwa ni pamoja na mashine ya umeme ya kutobolea mifupa (electric drilling machine), vifaa vya kukatia miguu (Amputation set) ,vifaa vya kuwekea vyuma kwa mgonjwa aliyevunjika,set za plate ndogo na kubwa za kuwekea vyuma ndani ya mfupa, . Vitanda vya wagonjwa wa mifupa (Orthopaedic beds) pamoja na Set za antena (external fixator).

Tazama Hapa>>>