HUDUMA YA UCHUJAJI DAMU NI HUDUMA MPITO ITOLEWAYO KWA WAGONJWA WENYE MATATIZO YA FIGO KUSHINDWA KUFANYA KAZI
Posted on: March 13th, 2024Mkuu wa Wilaya ya Tarime Mhe, Kanali Maulid Hassan Surumbu amesema huduma ya uchujaji damu ni huduma ya mpito kwa wagonjwa wenye matatizo ya figo kushindwa kufanya kazi hivyo kuhitaji msaada wa mashine maalum ya kusafisha au upandikizaji wa figo.
Mhe, Surumbu amesema hayo wakati akisoma hotuba ya Waziri wa afya Mhe, Ummy Mwalimu leo Machi 14, 2024 katika Maadhimisho ya Siku ya Figo Duniani akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe, Said Mohamed Mtanda.
“Huduma ya kuchuja Damu ni huduma mpito kwa wagonjwa wenye matatizo ya figo kushindwa kufanya kazi katika hatua hii figo ushindwa kazi au kuwa na uwezo mdogo wa kusafisha taka mwili hivyo kuhitaji msaada wa mashine maalum ya usafishaji au upandikizaji wa figo” Amesema Mhe Surumbu
Aidha Mhe, Surumbu amesema tafiti zinaonyesha kuwa watu milioni 850 usumbuliwa na tatizo la figo duniani na makadirio kwa watu waishio kusini mwa jangwa la sahara zinaonekana kuwa takribani ya watu 16 kati ya 100 wameathirika na tatizo la figo nakwa nchini Tanzania tafiti zinaonyesha kati ya asilimia 7% hadi 14% ya watanzania ambao ni wastani wa watu 10 kati ya 100 wanaathiriwa na ugonjwa wa figo.
Kwa upande wa Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara Dkt, Osmund Dyegura akitoa taarifa ya huduma ya magonjwa ya figo Hospitali ya Rufaa ya Mkoa amesema katika jitahada za serikali za kuongeza upatikanaji wa huduma za afya nchini kuanzia mwaka 2021 Wizara ya Afya iliweza kuanzisha Kliniki Maalum ya uchujaji Damu.
“Katika jitihada za serikali kuongeza upatikanaji wa huduma nchini kuanzia mwaka 2021 Wizara ya afya iliweza kuanzisha Kliniki maalum ya kuchuja Damu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara na wakati inaanza ilianza kuhudumia mteja mmoja lakini hadi sasa imeshaweza kuhudumia wateja zaidi ya 80”
Kwa upande wa mwakilishi wa chama cha wataalam wa figo nchini na wadau mbalimbali wa maswala ya Figo Dr. Sabina Mtulo Mmbali amesema lengo kubwa la wadau ni kuboresha huduma ikiwemo za uchujaji Damu.
Ameongezea kuwa huduma za uchujaji damu zimeenea sehemu nyingi za nchi ikiwemo Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara.