HOSPITALI YA RUFAA YA MKOA WA MARA YAPOKEA VIFAA TIBA KUTOKA WAZARA YA AFYA.
Posted on: September 16th, 2021Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto kupitia kampuni ya Philips Health care inayojihusisha na uuzaji na usambazaji wa vifaa tiba Leo Septemba 17, 2021 imekabidhi vifaa tiba vinavyokadiriwa kuwa na thamani ya takribani shilingi billion moja katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara ikiwa ni mpango wa Wizara kuhakikisha inaboresha miundombinu ya afya na kuimarisha upatikanaji wa Huduma bora katika hospitali za Rufaa za Mikoa.
Akizungumza wakati wa kukabidhi vifaa hivyo Mhandisi Damian S. Mbonabucha kutoka kampuni ya Philips kitengo cha vifaa Tiba amesema kuwa,Wizara imetoa vifaa hivi ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora katika maeneo ya karibu na kupunguza gharama za matibabu hivyo watahakikisha vifaa hivyo vinafungwa haraka na kuanza kutoa huduma iliyokusudiwa.
“Mtapokea vifaa vikiwa vinafanya kazi kwa kuwa tulijipanga kuvileta,kuvifunga na tutaondoka pale tuu mtakapojiridhisha vifaa vyote vinafanya kazi,alisema mhandisi Damiani”.
Aidha,Mhandisi Damian amesema baada ya kufunga vifaa hivyo watawajengea uwezo watumishi kwa kutoa mafunzo ya namna ya kutumia vifaa hivyo ili pindi wanapoondoka tayari viwe vimeanza kutumika na viendelee kutumika
Awali akipokea vifaa hivyo Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara Dkt.Elius Godfrey ameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto kwa kuona umuhimu wa kutoa vifaa hivyo kwani vitasaidia kwa kiasi kikubwa kuendelea kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi wa Mkoa wa Mara na maeneo ya Jirani.
Amesema miongoni mwa vifaa vilivyotolewa ni pamoja na vifaa kwa ajili ya uchomaji wa taka,vifaa vya kusaidia wagonjwa kupumua,vitanda vya kujifungulia,vitanda vya wagonjwa,mashine za mionzi,taa kwa ajili ya kusaidia Watoto wenye manjano,mashine ya kukata na kukausha bila kumwaga damu wakati wa upasuaji,vifaa vya usingizi pamoja na vifaa vingine.