Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere - Mara

HOSPITALI YA RUFAA MARA YAPOKEA MACHINE ZA KUSAFISHA FIGO (DIALYSIS MACHINE)

Posted on: July 26th, 2020

Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara, Imepokea mashine tisa (9)za kisasa kwa ajili ya huduma ya usafishaji wa figo kutoka Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na watoto ikiwa ni mkakati wa serikali kuziwezesha hospitali za Rufaa za Mikoa kutoa huduma hiyo.

Akizungumza wakati wa kupokea mashine hizo Mkuu wa Mkoa wa Mara Mh.Adam Malima amesema kuwa,kupatikana kwa mashine hizi zenye thamani ya Zaidi ya shilingi milioni mia tatu (300) kutaondoa adha na gharama kubwa  kwa wananchi wa Mkoa wa Mara kufuata huduma za matibabu katika hospitali ya kanda Bugando au hospitali ya Taifa muhimbili.

“Nitoe pongezi kwa serikali kuamua kuleta mashine hizi katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara,wananchi badala ya kwenda mbali watahudumiwa ndani ya Mkoa ambapo gharama zitapungua na mgonjwa atahudumiwa kwa shilingi 1,8000 tofauti na nchi jirani kama Kenya ambapo huduma hii inapatikana kwa gharama kubwa. Hili ni jambo la kujivunia kuona serikali yetu inaendelea kuimarisha huduma za afya katika Mkoa wetu.”

Katika hatua nyingine,Malima amehimiza Shirika la Nyumba la Taifa(NHC) ambao ni wakandarasi wa ujenzi wa hospitali ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere –Kwangwa ambapo Hospitali ya rufaa inatarajiwa kuhamia hapo kuhakikisha wanafanya kazi usiku na mchana  kukamilisha WING C ili  kitengo cha mama na mtoto pamoja na huduma za usafishaji wa figo  kuanza mapema  mwezi Agosti mwaka huu.

Kwa upande wake Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara Dkt. Joackim Eyembe amesema, miaka kadhaa iliyopita wananchi walilazimika kwenda India kufuata matibabu hayo,lakini kuletwa kwa mashine hizi ni neema kubwa kwa kuwa wananchi watahudumiwa ndani ya Mkoa na kutapunguza gharama kwao na kwa serikali.

“Sisi kupokea mashine  hizi tumepiga hatua kubwa za kiufanisi kwa kuwa kuwepo kwa huduma hii kutaokoa maisha ya wanachi wengi ikiwemo akina mama wengi pindi wanapojifungua na kutoka damu nyingi njia pekee ya kuokoa maisha yao ni kuwapatia huduma hii.”

Nae mratibu wa magonjwa yasiyo ya kuambukizwa kutoka wizara ya Afya Maendeleo ya Jami, Jinsia, Wazee na Watoto Bwn.Shadrack Buswelu amesema kuwa,Mkoa wa Mara umekuwa miongoni mwa Mikoa ya Tanzaniia Bara ambayo imepata  mgao wa mashine hizi zilizotolewa na serikali kupitia ufadhili wa serikali ya Falme za Kiarabu pamoja na Shirika la Fresinius German huku akiongeza kusema hospitali tayari ina wataalamu saba (7) waliopatiwa mafunzo hivyo huduma zitaanza kutolewa mapema pindi zoezi la ufungaji wa mashine hizo utakapokamilika.

“Amesema,Tumepokea jumla ya mashine 62 kutoka Fresinius Germany ambapo kati ya mashine hizo 17 tumezipeleka Zanzibar na 45 tumezipeleka katika hospitali mbalimbalia nchini ili kusaidia matibabu ya figo kwa wananchi wa Mikoa hiyo na matarajio ifikapo November Mwaka huu Mikoa 20 hapa nchini itakuwa ikitoa huduma hii hivyo wananchi watatibiwa ndani ya nchi na hawatapata taabu ya kufuata huduma hii mahali pengine.

Ameongeza kuwa mpaka sasa kuna Zaidi ya wagonjwa 1300 wanaofanyiwa matibabu ya figo ambapo ametaja vyanzo vya ugonjwa huu ni kuongezeka kwa magonjwa yasiyo ya kuambukizwa kama ugonjwa wa sukari,moyo, shinikizo la damu pamoja na utumiaji wa pombe uliokithiri,uvutaji sigara na utumiaji wa vyakula visivyofaa huku akiitaka jamii kuzingatia kanuni bora za afya ikiwemo kufanya mazoezi,kula vyakula kwa mpangilio na kuacha utumiaji uliokithiri wa pombe na sigara.

Sambamba na hilo kwa niaba ya wananchi wa Mkoa wa Mara,mhe.Mkuu wa Mkoa ametoa salamu za rambirambi kwa  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.John Pombe Magufuli na watanzania wote kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tatu Mhe.Benjamin William Mkapa,na  kuwataka watanzania wote kuwa watulivu katika kipindi hiki cha maombolezo huku akihimiza   kuishi tukienzi misingi ya uzalendo,mshikamano,uwajibikaji na utawala bora  ili tuijenge Tanzania mpya.