HOSPITALI YA RUFAA MARA YAPOKEA MACHINE YA KISASA YA X-RAY
Posted on: April 14th, 2020HOSPITALI YA RUFAA MARA YAPOKEA MASHINE YA KISASA YA X-RAY
Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara, Leo imepokea mashine ya kisasa ya X-Ray (Digital X-Ray) kutoka Wizara ya Afya Maendeleo ya jamii Jinsia Wazee na watoto kwa ajili ya kurahisisha na kuboresha utoaji wa huduma ya Mionzi katika hospitali za Rufaa nchini.
Akipokea mashine hiyo Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara Dr. Joachim Eyembe amesema kuwa,upatikanaji wa mashine hii ya kisasa kutaongeza ufanisi wa kazi kwa sababu machine hii ni bora Zaidi kuliko ile ya Analojia kwa kuwa ina uwezo wa kupiga picha zenye ubora wa hali ya juu na kuchunguza sehemu yeyote ya mwili wa binadamu.
Ameongeza kusema kuwa, mashine hii itasaidia kwa kiasi kikubwa kuhudumia wagonjwa wengi kwa muda mchache kwa sababu uwezo wake wa kutoa majibu ni muda mfupi takribani dakika kumi na tano(15), hivyo kwa siku ina uwezo wa kuhudumia wagonjwa mia moja(100).
Sambamba na hilo Dr.Eyembe ameishukuru serikali ya awamu ya tano kupitia Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii,Jinsia Wazee na Watoto kuona umuhimu wa kuboresha huduma za afya kwa kuleta vifaa tiba vya kisasa katika hospitali za Rufaa ambavyo vinasaidia kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa huduma bora za afya za wananchi.
Pia ameishukuru Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara chini ya uongozi wa Mhe. Adam Kighoma Malima kwa kuwa mstari wa mbele katika kufuatilia na kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora za afya pamoja na vifaa tiba katika Mkoa wa Mara unapewa kipaumbele na wananchi wa Mkoa wa Mara wanapata huduma bora za vipimo na matibabu.