Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere - Mara

HOSPITALI YA MWALIMU NYERERE YAANZA KUTOA HUDUMA

Posted on: August 30th, 2020

Hospitali ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere-Kwangwa leo,imeanza kutoa huduma za matibabu kitengo cha mama na mtoto kwa mara ya kwanza tangu ujenzi wake ulipoanza takribani Zaidi ya  miaka 40 iliyopita.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa huduma hizo Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Adamu Malima ameipongeza serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dk.John Pombe Magufuli kwa kuona umuhimu wa kumalizia ujenzi wa hospitali hii uliokwama ili kuienzi ndoto ya muasisi wa Hospitali hii hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

“Leo ni siku maalumu na ya furaha kuona ujenzi wa hospitali hii umekamilika na wananchi wa mkoa wa Mara wameanza rasmi kupata huduma za mama na mtoto mahali hapa”.

Mhe.Malima  ameongeza kusema kuwa uthubutu ni jambo  la msingi na muhimu katika kuleta maendeleo yeyote yale,hivyo kukamilika kwa kwa hospitali hii ni uthubutu pamoja na utekelezaji uliofanywa na viongozi wetu wa ngazi za juu na leo tunaona matunda yake ya kuanza kupata huduma za mama na matoto katika hospitali ambayo ilisahaulika miaka mingi.

Sambamba na hayo Mkuu wa mkoa amesema kuwa matarajio ya sasa baada ya huduma hizi ni kuanza kwa kitengo cha kusafisha figo pamoja na huduma za upasuaji ambapo amesema kuwa vifaa vyote tayari vimeshafungwa kinachosubiriwa ni kifaa maalumu kwa ajili ya kuthibiti umeme{stabilizer} na huduma kuanza kutolewa.

Kwa upande wake Mganga Mfawidhi wa hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara Dr.Joachim Eyembe,ameishukuru serikali ya Awamu ya Tano kwa juhudi na jitihada walizozionesha katika kuhakikisha hospitali hii inakamilika kwa wakati ikiwemo kubadilisha mjenzi wa awali TBA na kumpa kazi hii Shirika la Nyumba la Taifa NHC ambao wamefanya kazi kwa ufanisi mkubwa na hatimae Jengo limekamilika na huduma zimeanza kutolewa.

Nae Mkurugenzi Mkuu wa shirika la Nyumba la Taifa Ndg.Maulidi Banyani amesema ushirikiano uliofanya na viongozi katika kusimamia na kuhakikisha kazi zinafanyika ndio uliosababisha leo kazi ya ujenzi kukamilika na wananchi kuanza kupata huduma hivyo amehimiza  kudumisha ushirikiano na umoja katika kufanya kazi.

Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi Bi.Mary Makondo ameishukuru serikali kwa ushirikiano inaouonesha katika kuboresha huduma za afya kwa wananchi,pia  uongozi wa Mkoa wa Mara kwa usimamizi madhubuti kuhakikisha ujenzi unafanyika kwa kiwango kinachotakiwa na kukamilika kwa wakati.

Vilevile amemshukuru Mwenyezi Mungu kwa Baraka ya watoto watatu kuzaliwa siku hii ya uzinduzi wa huduma ya mama na mtoto ambapo mmoja kati ya watoto hao ameitwa jina la Julius kama heshima na ishara ya kumuenzi  muanzilishi wa hospitali hii  Hayati baba wa Taifa Mwl.Julius Kambarage Nyerere.

Bi Lucy Busala ni mama wa kwanza kujifungua katika hospitali hii na kumpa mtoto wake jina la Julius kama ishara ya kumuenzi Hayati Baba wa Taifa amesema kuwa ana furaha kubwa sana kuona huduma zimeanza kutolewa na yeye kuwa mama wa kwanza kujifungua mahali hapo hana budu kuishukuru serikali kwa kujali wananchi wake hususani akinamama kwa kuwaboreshea huduma za Afya.

“Nimekuja hapa mida ya saa mbili kijifungua,namshukuru Mungu nimejifungua salama na kupatiwa huduma nzuri hivyo napenda kumshukuru Rais John Pombe Magufuli kwa kutuboreshea

huduma.