Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere - Mara

CHANJO YA UVIKO 19 YAHITAJI ELIMU ENDELEVU - DKT.GWAJIMA

Posted on: August 15th, 2021

Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Mhe. Dorothy Gwajima  ametoa ufafanuzi kuhusu umuhimu wa chanjo na matumizi ya tiba asili kwa ajili ya  kuongeza kinga za miili.

Dkt.Gwajima ameeleza hayo akiwa katika ziara ya kukagua hali ya utoaji huduma za afya na shughuli za maendeleo ya Jamii katika Mkoa wa Mara Agosti 16 Mwaka huu.

Dkt. Gwajima amesema kuwa,pamoja na juhudi kubwa zinazofanywa na serikali kuelimisha wananchi kuhusu UVIKO 19 na namna ya kujikinga ikiwemo matumizi ya tiba asili na Chanjo kwa sasa bado kuna watu wasio na nia njema wanarudisha nyuma jitihada hizi katika mapambano ya kuutokomeza ugonjwa huu.

Amesema,Elimu endelevu inapaswa kutolewa kuhusu matumizi ya tiba asili pamoja na huduma ya chanjo inayoendelea kutolewa nchini ili isaidie jamii kuwa na uelewa na kufanya maamuzi kwa hiari yao kuchanja ili kujikinga na janga la UVIKO 19 linalosumbua ulimwengu na kuacha kuamini maneno ya upotoshaji na uzushi yanayoendelea kutolewa na watu wasio na nia njema.

“Hata darasani  haiwezekani wanafunzi wote wakapata alama inayofanana,kuna watakaopata asilimia 80 na wengine asilimia 30 lakini kuna kundi hata ukifanya nini watafeli tuu  mpaka wapatiwe twisheni na vipindi vya ziada ndio wataelewa,hivyo hata suala la Chanjo ya UVIKO 19 lipo hivyo,hakuna haja ya kutumia nguvu tuendele kutoa elimu endelevu na pia wananchi msiwe wepesi kudanganywa tumini mtandao kujifunza faida za chanjo”alisema Mhe.Gwajima

Aliendelea kusema kuwa,Mwaka jana UVIKO ulivyoingia  hapa nchini Chanjo haikuwepo,Hivyo Hayati Dkt.John Pombe Magufuli  akiwa Chato alisema tutumie tiba asili kujifukiza kama njia mbadala ya kujikinga hivyo tiba asili ipo,ilikuwepo na inaendelea kutumika na wananchi waache kuaminishwa mambo yasiyo na ukweli.

Amesema,sijutii kuhimiza matumizi ya tiba asili na uhamasishaji wote uliofanyika  ni halali kwa mujibu wa Sheria ya tiba asili na Tiba Mbadala Na 23 ya  Mwaka 2002,hivyo ujio wa chanjo ya UVIKO 19 haujazuia matumizi ya tiba asili bali vinasaidiana huku Chanjo ikiwa kinga ya kisasa Zaidi tusipotoshane.

“Katika hotuba ya Hayati dkt John Pombe Magufuli akiwa Chato Januari 27 mwaka huu hakuzuia Matumizi ya chanjo bali alisema serikali isikimbilie kuingiza chanjo pasipo kujiridhisha na ndicho kilichofanyika, serikali  chini ya Rais Samia Suluhu Hasan imejiridhisha na usalama wa chanjo na kushauri wananchi kuanzia miaka 18 wajitokeze kuchanja ili kujikinga na maradhi hayo.

Dkt.Gwajima ametoa rai kwa wananchi kuendelea kusikiliza ushauri unaotolewa na wataalamu wa afya na kupata chanjo itakayowasaidia kunusuru afya zao na kubainisha kuwa kwenye baadhi ya nchi ugonjwa wa UVIKO 19 umeanza kuwapata watoto jambo ambalo linaweza kuleta madhara Zaidi hivyo hatua zote za kujikinga inabidi ziwekewe mkazo na kufuatwa.

Awali akitoa taarifa ya hali ya Afya katika Mkoa wa Mara kwa Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto,Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mara dkt. Juma Mfanga amesema kuwa,mwitikio wa chanjo katika Mkoa wa Mara ni Mzuri kwani tangu kuzinduliwa kwa zoezi la uchanjaji Agosti 5  jumla ya watu 4856 wamechanjwa

Amesema Mkoa unaendelea kujitahidi kuhakikisha kuwa kila anayehitaji chanjo anapatiwa huduma hiyo kwa ukaribu Zaidi ambapo amebainisha  vituo vya kutolea chanjo vimeongezwa kutoka 22 vya awali hadi vituo 34 kwa sasa.

Hata hivyo taarifa zinaonesha kuwa idadi ya wagonjwa wengi wanaoongoza kwa kuugua,kulazwa na kutumia mashine ya oksijeni katika hospitali ni wale wasiochanja,hivyo watanzania wanapaswa kubadilika na kuachana na taarifa za kupotosha zinazotolewa na watu waso na nia njema.