Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere - Mara

BODI YA ZABUNI YA HOSPITALI YAZINDULIWA RASMI

Posted on: April 30th, 2020

Bodi ya Zabuni ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara imezinduliwa Rasmi jana terehe 29/04/2020 na Mganga Mfawidhi wa Hospitali Dr Joachim Eyembe ambae pia ndio Afisa Masuuli wa  Hospitali ikiwa ni baada ya Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kuteua Bodi za Zabuni na Sekretarieti(PMU) zake katika Hospitali zote za Rufaa za Mikoa nchini.

Akizungumza wakati akizindua Bodi hiyo, Mganga Mfawidhi aliwapongeza Wajumbe wa Bodi na Sekretarieti kwa Uteuzi huo na kwa kubahatika kuwa wajumbe wa kwanza wa Bodi ya kwanza ya Manunuzi ya Hospitali na kuwataka kufuata na kusimamia sheria ya manunuzi ya umma ipasavyo kwani kutokujua sharia hakutoi uhuru wa kutowajibishwa nayo. Lakini pia akatoa angalizo la kutokutumia sheria hiyo kukandamiza maslahi ya Hospitali na Serikali kwa Ujumla.

Aidha Dr Eyembe amesisitiza swala la kuzingatia misingi na maadili ya ununuzi wa umma kama yalivyo bainishwa katika Sheria ya Ununuzi wa Umma Na. 7 ya mwaka 2011 pamoja na marekebisho yake ya mwaka 2013. Dr Eyembe akawasihi wajumbe kuzingatia zaidi swala la usiri katika kutekeleza majuku yao na kujiepusha na vitendo vya rushwa kwani majukumu waliyopewa yanavishawishi vingi vya upokea rushwa.

Wajumbe nao wamemshukuru Mganga Mfawidhi kwa niaba ya Katibu Mkuu kwa Uteuzi huo na kuahidi kutekeleza majukumu yao kama inavyotakiwa huku wakitanguliza maslahi ya Hospitali na serikali kwa ujumla mbele. Pia Wajumbe wa Bodi ya Zabuni wameitaka Sekretarieti yake kuisaidia bodi kikamilifu katika kufanya maamuzi sahihi lakini kwa kufuata sheria, miongozo, kanunuzi na taratibu za ununuzi wa umma kwani sekretarieti ndio hasa mratibu mkuu wa manunuzi yote ya Hospitali.

Awali kabla ya Uzinduzi huo, Sekretarieti ya Bodi ya Zabuni ya Hospitali ikishirikiana na Mkuu wa Kitengo cha Ununuzi na Ugavi toka Ofisi ya Katibu Tawala Mkoa wa Mara Bi Stela J. Sangayau, iliwapitisha wajumbe katika baadhi ya vifungu vya Sheria ya Ununuzi wa Umma Na. 7 ya mwaka 2011 na Kanuni zake za Mwaka 2013 ili kuwapa wajumbe muongozo juu ya majukumu yao katika manunuzi ya umma.