Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere - Mara

BILIONI 9 YATENGWA KUMALIZIA UJENZI WA HOSPITALI YA RUFAA YA KUMBUKUMBU YA MWALIMU NYERERE

Posted on: August 15th, 2021

Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima amesema kuwa serikali imetenga fedha  kiasi cha shilingi bilioni 9 kwa ajili ya kuendelea kumalizia ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere iliyopo kata ya Kwangwa  katika Manispaa ya Musoma ambayo Ujenzi wake umefikia asilimia 75 huku huduma za mama na mtoto pamoja na kusafisha Figo yaani dialysis zikiwa zimeanza kutolewa.


Dkt.Gwajima amtoa kauli hiyo leo tarehe 16/8/2021 alipotembelea haspitali hiyo  akiwa katika ziara ya kukagua hali ya utoaji wa huduma za afya na shughuli za maendeleo ya jamii Mkoani Mara


“Serikali ya awamu ya sita chini ya  Rais Samia Suluhu Hasan imetenga kiasi cha shilingi bil. 9 kwa ajili ya kuendelea kumalizia ujenzi wa Hospitali hii hivyo niwaombe wakandarasi fedha hizi zitumike haraka kukamilisha Wing A’ili huduma za wagonjwa wa nje {OPD},Huduma za dharura na maabara zianze kufanya kazi”amesema dkt. Gwajima.


Amesema, dhamira ya serikali ni kuifanya hospitali hiyo isaidie kwa kiwango kikubwa katika utoaji wa huduma za kibingwa za mifupa na kusafisha Figo ili  kupunguza mlindikano wa wagonjwa wanaopata huduma hizo katika  Hospitali ya Taifa Muhimbili na Benjamin Mkapa.


Aidha dkt. Gwajima ameupongeza uongozi wa hospitali kwa juhudi walizofanya za kuanzisha huduma ya kusafisha figo kwani ni mafanikio makubwa sababu huduma hiyo ni muhimu sana na itapunguza gharama kwa wagojwa kwenda kutibiwa mbali huku akisisitiza juhudi Zaidi zifanyike ilihapo baadae huduma iboreshwe na wagonjwa waweze kupandikizwa Figo hapahapa nchini badala ya kwenda India ama nchi zingine.


Awali akimkaribisha Waziri wa Afya ,Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Dkt. Joachim Eyembe amesema tangu Hospitali hiyo ianze kutoa huduma mwezi Agosti Mwaka Jana Zaidi ya Akinamama 1950 wameweza kujifungua katika hospitali huku huduma ya kusafisha Figo ilianza kutolewa tarehe 4 Agosti mwaka huu.


Dkt Eyembe amesema pamoja kazi nzuri wanayoifanya ya kutoa huduma kwa wananchi bado Hospitali hiyo inakabliliwa na changamoto wa uhaba wa madktari Bingwa kwani waliopo sasa ni wanne tu pamoja na Nyumba za watumishi huku akibainisha mkakati wa kutatua changamoto ya watumishi ni  kupeleka madaktari wane kusoma ili waje kusaidia utatuzi wa changamoto hiyo na kuleta mapinduzi chanya ya huduma za Kibingwa.


Kuhusiana na suala la kukabiliana na Uviko 19 Dkt. Gwajima amewataka watumishi wa afya pamoja na wananchi kuchoma chanjo ya UVIKO -19 kwani ni salama na haina madhara yeyote kwa Binadamu na kuachana na habari za uzushi zinazosambazwa mitandaoni kuhusu chanjo badala yake watumie mitandao ya kijamii kupata elimu na takwimu sahihi itakayowasaidia.


“Watu wengi wanaolazwa na kutumia oxygen ni ambao hawajachanja,chanjo ni salama,uzushi na upotoshaji unaotolewa na baadhi wa watu wenye nia ovu upuuzwe kwani chanjo zote zinatolewa nje hakuna chanjo tunayoitengenezwa Tanzania.alisema Gwajima


Serikali imejiridhisha na chanjo inayotolewa hivyo wananchi waondoe hofu na kuchanja huku wakiendelea kuchukua tahadhari za kujikinga kupata maambukizi kama kufanya mazoezi,kula mlo kamili,kuvaa barakoa na kunawa mikono kwani chanjo hii haizuii kupata maambukizi bali inasaidia kuimarisha kinga ya mwili na kuzuia Corona kali.