ZIARA YA KATIBU WA ITIKADI NA UENEZI WA CHAMA CHA MAPINDUZI TAIFA KATIKA HOSPITALI YA MNMRRH
Posted on: May 14th, 2026Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi Ndg. Kenani Kiongosi amefanya ziara ya kutembelea maendeleo ya mradi wa ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere leo tarehe 14/05/2026.
Ndg.Kenani amesema Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere ni mradi ambao ni mkombozi kwa wananchi wa mkoa wa Mara na maeneo ya jirani. Aidha, amewashukuru watumishi wa hospitali kwa kufanya kazi nzuri.
“Watumishi Mungu azidi kuwalinda, nimezunguka na kuongea na wagonjwa waliolazwa wodini hakika wanafurahia huduma mnazotoa pia endeleni kufanya kazi kwa moyo huo huo lakini mkumbuke kuishi” amesema Ndg. Kenani Kiongosi
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi amesema mradi wa ujenzi wa hospitali ya mkoa wa Mara ni fikra za baba wa Taifa letu Mwalimu Julius K. Nyerere hivyo kukamilika kwa mradi wa hospitali itakuwa ni kukamilisha fikra za baba wa Taifa.
Aidha, amewataka watumishi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere na wananchi wa mkoa wa Mara kutunza miundombinu “hii miundombinu ni ya kwetu hivyo kila mmoja wetu anawajibika kuitunza na kuilinda, endapo miundombinu ikiharibiwa wananchi wa mkoa wa Mara mtakuwa waathirika wakubwa kwa kukosa huduma za afya”
Nae mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Mtambi amesema viongozi wa Chama Chama Mapinduzi wanapokuja kufanya ziara ya miradi ni njia ya kufatilia utekelezaji wa ilani ya Chama Cha Mapinduzi na hivyo kama serikali wanafanya kazi ya kuhakikisha mkataba walioingia na wananchi unafanyiwa kazi. Aidha, Mhe. Evans Mtambi amesema Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara inatoa huduma bora kwa wananchi wa Mara na maeneo ya jirani pia imepunguza gharama kwa wananchi za Kwenda hospitali ya Kanda ya Bugando.



