Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere - Mara

WATUMISHI MARA WAPEWA MAFUNZO KUKABILIANA NA VIRUSI VYA CORONA

Posted on: March 19th, 2020

Watumishi wa idara ya Afya pamoja na sekta zinazohudumia wageni Mkoa wa Mara wanapatiwa mafunzo ya kuwajengea uwezo wa kukabiliana na magonjwa ya milipuko ikiwemo virusi vya ugonjwa wa  corona (COVIC-19).Mafunzo hayo yameanza kufanyika leo tarehe 19/3/2020 katika chuo cha matibabu Musoma COTC kilichopo manispaa ya Musoma.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mara Dkt. Florian Tinuga amesema kuwa Lengo la  mafunzo hayo ni kujengeana uwezo wa namna bora ya kuweza kukabiliana na magonjwa ya milipuko ikiwemo yatokanayo na  virusi vya corona.

Dkt. Florian Ameongeza kuwa mafunzo haya yatawajengea uwezo watumishi kujiamini na kuondoa hofu ili waweze kuwahudumia wananchi ipasavyo.

“Tunataka mafunzo haya yawe ndio msingi wa kukabiliana na dharula zote za afya katika Mkoa na baada ya mafunzo natarajia  matokeo yake watumishi waweze kujiamini,wawe na ujuzi ili tuweze kuandaa timu ambayo itaweza kukabiliana na majanga yote ya milipuko katika Mkoa wetu”.

Kwa upande wake Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara Bwana Method B. Mkoba amewataka watumishi wote wanaopatiwa mafunzo kuzingatia mafunzo hayo ili waweze kuyatekeleza kwa ufanisi na kuwa mstari wa mbele kufikisha elimu sahihi kwa wananchi na kuwaondolea hofu waliyonayo.

Aidha amewatoa hofu wananchi wote wa Mkoa wa Mara kuwa kwa sasa mkoa upo salama  na kuwasisitiza waondoe shaka maana serikali imejipanga ipasavyo kukabiliana na mlipiko huu wa virusi vya corona, na Zaidi waachane na mambo ya uvumi bali wafuate maelekezo kadri yanavyotolewa na serikali.

Katibu tawala pia ameipongeza Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto kwa juhudi na jitihada wanazozifanya kukabiliana na mlipuko huu tangu ulivyotokea.

“Serikali inafanya kazi kubwa kukabiliana na mlipuko wa virusi vya corona hususani kutoa elimu kwa wananchi,kutoa taarifa za kila hatua inayochukua pamoja na tahadhari kwa wananchi namna  ya kujikinga na ugonjwa huu”.

Wakati Huohuo Mtaalamu wa magonjwa ya Milipuko Dkt. William Nangi ameeleza kuwa mafunzo hayo ni muhimu sana hususani katika maeneo yaliyopo pembezoni wa mipaka ambapo ni rahisi  kuambukizwa kutokana na muingiliano wa watu toka nchi jirani.

“Tunatoa mafunzo haya ili kuwaandaa na kuwajengea uwezo wa kuwahudumia wagonjwa wa mlipuko wa Virusi vya Corona pamoja na kutoa elimu sahihi kwa wananchi kuhusu kujikinga na maambukizi”.

Mafunzo haya yanatolewa kwa muda wa siku nne(4) na wataalamu kutoka Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,  Wazee na  Watoto na kujumuisha wataalamu wa Afya Mkoa wa Mara,wataalamu kutoka viwanja vya ndege,Mmpaka wa Tanzania  na Kenya(Sirari), Hifadhi ya Taifa Serengeti pamoja na Wadau wa Afya.