Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere - Mara

WANANCHI MARA WAHIMIZWA KUCHOMA CHANJO YA UVIKO - 19

Posted on: August 6th, 2021

Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Ally Salum Hapi amewataka wananchi wa Mkoa wa Mara waliopo kwenye makundi   yaliyopewa kipaumbele kupatiwa  chanjo ya Uviko -19 kutumia fursa hii kuchanjwa chanjo hiyo kwani watalamu wa afya wamehakikisha kuwa chanjo hii ni salama na haina madhara yeyote kwa binadamu.Kauli hiyo ameitoa leo tarehe 5, Agosti 2021 wakati wa  uzinduzi wa uchanjaji wa chanjo ya Uviko – 19 katika Mkoa wa Mara lililofanyika katika viwanja vya ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara.

“Nipende kuwahakikishia wananchi kuwa wataalamu wetu wamefanya kazi kubwa kujiridhisha kuwa chanjo hii iko salama kama chanjo zingine ambazo tayari tumeshapatiwa  kama chanjo ya surua,polio na Homa ya ini”alisema Mheshimiwa HapiAmesema Wananchi mnapaswa kuondoa hofu na kuacha kusikia maneno ya mtaani yanayopotosha badala yake fuateni ushauri unaotolewa na watalamu wa afya kuwa chanjo hii ni sawa na chanjo nyingine zozote ambazo tunapatiwa kwani hakuna chanjo ambayo inatengenezwa nchini hivyo suala la kusema chanjo hii sio salama ni upotoshaji.

Aidha Mheshimiwa Hapi amewataka wananchi kuendelea kuchukua tahadhari zote za kujikinga  dhidi ya Uviko - 19 kwani ugonjwa huu upo na watu wanapoteza maisha sababu ya ugonjwa huu.“Sisi tupo mpakani tunapakana na nchi ya kenya na uganda hivyo hatupo salama hivyo jambo hili sio la mzaha tuchukue tahadhari ikiwepo kuepuka mikusanyiko isiyo ya lazima,kuvaa barakoa na kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni.

Hapi ametumia nafasi hii kuzuia shughuli zote za mikusanyiko isiyo na kibali maalumu cha serikali  kwa kufuata muongozo wa Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii,Jinsia ,Wazee na Watoto unaolenga kupunguza kuenea kwa maambukizi ya uviko -19.“Mwongozo una mambo mazuri ambayo yakisimamiwa ipasavyo yatapunguza maambukizi mfano muongozo unataka harusi na shuhuli za misongamano kuahirishwa au kama zitafanyika iwe kwa muda mfupi, maeneo  ya wazi na watu wachache ambao wamechukua tahaadhari zote za kujikinga ikiwemo kuvaa barakoa.

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mara Dkt.Juma Mfanga amewahimiza wananchi kuondoa hofu na kuchanja chanjo hii kwani ni chanjo salama na inasaidia kufubaza makali ya virusi vya uviko – 19 pindi inapotokea maambukizi.“Niwahimize ndugu zangu kuchoma chanjo hii kwani gharama za matibabu pindi upatapo ugonjwa huu ni kubwa sana ambapo kwa siku moja mtu anaweza kutumia mitungi ya gesi 3 – 5 jambo  linaloweza kupelekea kushindwa kumudu gharama za matibabu na kupoteza maisha.alisema dkt.Mfanga

Sambamba na hilo amesisitiza wananchi kuzingatia taratibu za kiafya zilizowekwa kujikinga na ugonjwa huu ikiwemo kujenga utamaduni wa kufanya mazoezi,kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni,kutumia vitakasa mikono na kuvaa barakoa.Aidha amebainisha makundi yaliyoweza kupewa kipaumbele kuchanja chanjo hii kuwa ni watumishi wa afya,watu wenye umri wa miaka 50 na Zaidi,watu wenye magonjwa sugu, na watumishi wa vyombo vya ulinzi na usalama.

Mkoa wa Mara umepokea jumla ya dozi elfu ishirini na tano(25) za chanjo na katika Manispaa ya Musoma huduma hii itatolewa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara pamoja na Kituo cha Afya Nyasho lakini hapo mbeleni kutaongezwa wigo kutokana na uhitaji wa watu wanavyozidi kuhamasika kuchanjwa.