Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere - Mara

UPATIKANAJI WA MAJI WASISITIZWA MAENEO YA KUTOLEA HUDUMA ZA AFYA.

Posted on: January 8th, 2021

Afisa Muuguzi kutoka Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Ndg, Edwin Damas ameushauri Uongozi wa hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara kuhakikisha maeneo yote ya kutolea huduma maji yanapatikana ili kujikinga na maambukizi ya magonjwa kwa watumishi, wagonjwa wanaowapatia huduma pamoja na jamii.

Ndg.Damas ameseme hayo Leo wakati akizungumza na watumishi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara ikiwa ni moja ya hatua ya kutoa mrejesho wa tathmini ya namna gani watumishi wanatoa huduma za afya kwa kuzingatia na kuzuia maambukizi kutoka kwa wagonjwa pamoja na wagonjwa kutopata maambukizi mengine kutoka mazingira ya kazi.

Amesema kuwa,katika eneo lolote lile la kutolea huduma ya afya lazima kuhakikisha kwamba maji yanapatikana muda wote kwa kuwa inasaidia kwa kiwango kikubwa kuweka mazingira katika hali ya usafi na kujikinga na maambukizi ya vimelea vya magonjwa mbalimbali.

Aidha amesema kuwa Kila Mtumishi anatakiwa kuzingatia hatua zote za kuweza kuzuia kupata maambukizi kwake binafsi, kwa wagonjwa anaowahudumia pamoja na jamii wakati wa kutoa huduma na ili jambo hilo lifanikiwe ametoa wito kwa watumishi wote kuchukua tahadhari kwa kutambua kuwa kila anayekuja hospitali anaweza kuwa na mambukizi hivyo wazingatie kutumia vifaa vya kujikinga pale inapobidi na pia wananchi wahakikishe wanasafisha mikono yao pindi wanapoingia na kutoka katika mazingira ya hospitali ili kuepusha kubeba vimelea vya magonjwa.

Sambamba na hayo ameupongeza Uongozi wa hospital pamoja na  watumishi kwa kutoa huduma iliyo bora kwa wananchi na pia kuwa na uelewa mzuri  juu ya namna bora ya kujikinga na maambukizi kwao binafsi,kuwakinga wagonjwa wanaowahudumia pamoja na kuweka mazingira ya kutolea huduma.