Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere - Mara

TANNA MARA - WAUGUZI FANYENI KAZI KWA KUZINGATIA MAADILI NA MIIKO YA UUGUZI

Posted on: May 20th, 2021

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mara Dkt.Frolian Tinuga amewataka wauguzi wa Mkoa wa Mara kufanya kazi kwa bidii na  weledi kwa kuzingatia miiko na maadili ya taaluma  katika kuhudumia wagonjwa ili kuweza kuboresha huduma za Afya katika Mkoa.


Dkt.Tinuga  ametoa kauli hiyo  wakati akifungua Mkutano wa  chama Cha Wauguzi, TANZANIA NATIONAL NURSES ASSOCIATION-TANNA Mkoa wa Mara kilichofanyika katika Halmashauri ya Wilaya ya Bunda lengo Ikiwa ni kujadili na kuweka mikakati madhubuti itakayosaidia kupunguza changamoto zinazokwamisha utoaji wa huduma Bora kwa wananchi.


''Niwahimize  Wauguzi mliopo katika kikao hiki  muendelee kuchapa kazi kwa kuzingatia miongozo  na taratibu za kiuguzi ili jamii ya wananchi tunaowahudumia waendelee kufurahia huduma tunayowapatia na kupunguza malalamiko yatokanayo na baadhi ya Wauguzi kutotenda vile taaluma ya kiuguzi inavyotaka


Amesema kuwa anatambua mchango wa wauguzi  katika jamii na anawapongeza kwa  kuendelea kutoa Huduma nzuri kwenye mazingira magumu lakini pamojana hayo ili kutekeleza majukumu ya kiuguzi kwa ufanisi ni lazima Wauguzi kufuata miongozo yote ya kitaaluma ikiwemo kuwa nadhifu maeneo ya kazi kwa kuvaa sare inayotakiwa,kuwa wabunifu katika utoaji huduma na kutumia lugha isiyo Kali kwa wagonjwa wanaohiitaji faraja.


Aidha amesisitiza kuwa mabaraza ya  kitaaluma yatumike katika kuonya na Kutoa maamuzi pale ambapo muuguzi atatuhumiwa kufanya Jambo kinyume Cha taaluma na maadili ya kazi yake.

 ''Nawasihi wauguzi kufanya kazi kwa ushirikiano na kujiunga na Chama Cha wauguzi ili pindi panatokea changamoto muweze kusaidika katika kutatua changamoto zitakazojitokeza kulingana na maadili ya taaluma.


Sambamba na hayo amewataka viongozi wa TANNA Mkoa pamoja na  Muuguzi Mkuu wa Mkoa wasimamie ipasavyo watu wa chini yao ili kusahihisha makosa yanayojitokeza katika utekelezaji wa majukumu yao Ikiwa ni pamoja na kufungua Tawi la TANNA kwa kila Halmashauri ili wauguzi wasaidike mahali walipo.