TAKRIBANI MITI 3,749 IMEPANDWA KATIKA SHAMBA LA MITI HOSPITALI YA RUFAA YA MKOA YA KUMBUKUMBU YA MWL. NYERERE
Posted on: July 30th, 2024Hayo yamesemwa na Meneja Wakala wa Huduma za Misitu(TFS) Wilaya ya Musoma Bw. Hamisi B. Kiberege wakati akisoma taarifa ya mradi wa upandaji miti kwa kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa bw. Godfrey Mnzava baada ya Mwenge wa Uhuru kuwasili katika shamba la miti Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere.
Bw. Hamisi B. Kiberege amesema kuwa mchakato wa upandaji miti katika eneo la Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere ulianza januari, 2023 na miti 3,749 ilipandwa katika eneo hilo.
“Mnamo Januari, 2023 mchakato wa upandaji miti katika eneo la Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere ulianza, miti 3,749 ilipandwa na miti 3,702 sawa na asilimia 98 ndiyo ilifanikiwa kukua” Amesema Bw. Hamisi B. Kiberege
Aidha, Bw. Hamisi B. Kiberege aliongezea kuwa mradi huu wa upandaji miti umegharimu kiasi cha shilingi 6,575,000 ambazo zimetolewa na uongozi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere.
Kwa upande wake kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa Bw. Godfrey Mnzava amesema kuwa utunzaji wa mazingira ni agenda moja wapo uliobeba ujumbe wa Mbio za Mwenge mwaka huu , hivyo mwenge umefika katika shamba hilo ili kuona jitihada za utunzaji mazingira kupitia upandaji wa miti.
Pia, Bw. Godfrey Mnzava ambaye ni kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa alipanda mti katika shamba hilo.
Kauli Mbiu ya Mwenge wa Uhuru 2024 “Tunza Mazingira na Shiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa Ujenzi wa Taifa Endelevu”