Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere - Mara

MARA YAWEKA MIKAKATI KUDHIBITI KIFUA KIKUU NA UKOMA

Posted on: January 18th, 2021

Mratibu wa Kifua Kikuu na Ukoma Mkoa wa Mara Dr.Fabian Byesigwa amewataka waganga wakuu wa Wilaya pamoja na Waratibu wa kifua Kikuu na Ukoma Mkoa wa Mara kuacha tabia ya kukaa ofisini na kusubiri kuletewa taarifa badala yake wanapaswa  kwenda kutembelea vituo vinavyotoa huduma ili kuona hali ya  utendaji kazi katika vituo hivyo na  namna gani wanaweza kusaidia kutatua changamoto zinazokwamisha juhudi  za kutokomeza maambukizi ya  Kifua Kikuu na Ukoma Mkoani Mara.

Dr. Byesigwa ametoa kauli hiyo jana wakati wa   kikao cha kupitia na kurekebisha Takwimu za Kifua Kikuu na Ukoma Mkoa wa Mara kinachofanyika kwa muda wa siku mbili katika ukumbi wa Uwekezaji Mjini Musoma na kujumuisha waganga wakuu wa Wilaya,Makatibu wa afya, waratibu wa kifua kikuu na ukoma Mkoa pamoja na wataalamu wa afya kutoka hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara.

Amesema kuwa,kuna haja ya Waganga wakuu wa Wilaya kuacha tabia ya  kukaa ofisini na kusubiri kuangalia taaarifa kwenye mfumo na kusahau wajibu wao kuwa wao ndio wasimamizi wa masuala yote ya afya katika Halmashauri na Wilaya,hivyo wanapaswa  kutembelea maeneo yote hatarishi yanayodhaniwa ni kisababishi cha maambukizi ya kifua kikuu ambapo kwa kufanya hivyo kutasaidia kujua mwenendo wa maambukizi ya ugonjwa na kuweza kufanya  tathmini sahihi ya namna gani mikakati ya kudhibiti Kifua Kikuu inaendana na mazingira halisi.

Amesema kuwa,Hali ya maambukizi ya kifua kikuu na Ukoma kwa sasa  kimkoa ni wastani lakini watumishi hawapaswi kuridhishwa na matokeo hayo badala yake waongeze bidii katika uwajibikaji kwa kuendelea kuibua wagonjwa na kuwapatia matibabu na pia kuhakikisha taarifa zote zinaingiza kwenye mfumo kwa usahihi ili ziweze kusaidia kuona wapi kuna changamoto na namna gani changamoto hizo zinaweza kutatuliwa kwa wakati.

Aidha ameongeza kusema kuwa madaktari wote wanapaswa kutumia weledi na taaluma zao vizuri katika kufanya uchunguzi kwa wagonjwa ili kuweza kupata majibu yenye tija yatakayosaidia  kuibua na kutoa matibabu stahiki kwa wagonjwa ili kupunguza kasi ya ueneaji na vifo vitokanavyo na Kifua Kikuu na Ukoma.

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Wilaya ya Butiama Dr. Suke ameshauri kuwa ili kuhakikisha tunadhibiti Kifua Kikuu lazima viongozi wote katika ngazi ya chini kutafuta mikakati endelevu ya kuthibiti Kifua Kikuu badala ya kusubiri maelekezo kutoka  ngazi za juu ambayo kwa namna moja ama ingine yanaweza yasitekelezeke kwa wakati kulingana na mazingira ya eneo husika.

Amesema,kifua kikuu  ni ugonjwa unaodumu kwa muda mrefu na kuua wagonjwa wengi japokuwa chanjo zipo na zinatolewa kwa wananchi, hivyo kama viongozi  tunapaswa tufanye ufuatiliaji wa kina kwa wagonjwa wanaoibuliwa na pia kufanyike tathmini ya huduma za uchunguzi zinazotolewa na madaktari kwa wagonjwa ili kujua chanzo hasa cha tatizo hili kuendelea kuwepo na namna gani tunalitatua.

Sambamba na hilo DR.Byesigwa ametoa wito kwa jamii pamoja na maduka ya dawa  binafsi kushiriki katika harakati za kutokomeza Ugonjwa huu kwa sababu Kifua Kikuu ni ugonjwa Unaotibika na pindi wanapoona mtu ana dalili za kifua kikuu basi ashauriwe kwenda katika vituo vya kutolea huduma za afya kwa uchunguzi na matibabu sahihi badala ya kujificha ama kutumia dawa pasipo ushauri wa wataalamu wa afya.