MARA YAAZIMIA KUBORESHA HUDUMA YA LISHE
Posted on: May 17th, 2021Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara Mhandisi Faustine Terai amewataka wajumbe wa kamati ya Lishe ya Mkoa wa Mara kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa ufanisi ili kuboresha utekelezaji wa Afya za Lishe zitakazopelekea Mkoa kufanya vizuri kitaifa kwa Mwaka 2021.
Mhandisi Terai ametoa kauli hiyo wakati akifungua kikao Cha kamati ya Lishe ya Mkoa wa Mara kilichokutana kujadili na kufanya tathmini ya utekelezaji wa afua za lishe,kikao kilichofanyika Jana tarehe 18 Mei 2021 katika Ukumbi wa Uwekezaji uliopo ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara
''Ninawaomba ndugu zangu wajumbe wa kamati hii na wataalamu wengine tuliopo hapa tujadili na kuweka mikakati madhubuti itakayotusaidia kupunguza changamoto zinazokwamisha utekelezaji wa afua za lishe na kurudisha Mkoa wetu nyuma ili hapo baadae Mkoa tuweze kufanya vizuri kitaifa.
Aidha amemtaka Mganga Mkuu wa Mkoa kuwasimamia kikamilifu Afisa lishe pamoja na wataalamu wengine katika utendaji kazi wao kwa kuibua na kutatua changamoto na mapungufu yanayojitokeza katika utekelezaji wa majukumu ikiwemo katika kadi alama lishe kwa kipindi Cha Nusu mwaka Julai Hadi Disemba 2022 ili wakati wa Tathmini Mkoa uweze kupata nafasi nzuri.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mara Dkt.Frolian Tinuga ameeleza kuwa, ukilinganisha mafanikio ya Mkoa katika masuala ya Lishe kwa kipindi Cha miaka ya nyuma na sasa Mkoa wa Mara umefanikiwa kupiga hatua kubwa sana katika utekelezaji na Uboreshaji wa afua za lishe kutoka kuwa nafasi za mwishoni Hadi nafasi ya 17 kitaifa.
''Amesema matokeo haya yanatokana na ushirikiano na juhudi kubwa zinazotolewa na wataalamu mbalimbali pamoja na viongozi wa Mkoa katika kutekeleza kikamilifu majukumu ya kuboresha Afya ya jamii,hivyo amewasihi watendaji wa lishe pale wanapokwama ama kukumbana na changamoto waweze kuomba msaada kwa watendaji wengine ili kuweza kuleta ufanisi katika utekelezaji wa masuala ya Lishe kwa wananchi wa Mkoa wa Mara.
Awali akitoa tathmini ya matokeo ya kadi alama lishe kwa Nusu mwaka 2021,Afisa lishe wa Mkoa wa Mara ndg Paul Makali alisema miongoni mwa viashiria vinavyopimwa ni pamoja na asilimia ya vikao vya lishe ngazi ya Halmashauri,usimamizi shirikishi,kaguzi za chakula pamoja na Akina mama wanaopatiwa ushauri wa ulishaji wa watoto kutoka kwa wahudumu wa Afya ngazi ya jamii.
Viashiria vingine ni utoaji wa matone ya vitamin A kwa watoto,Madini chuma kwa Akina mama wajawazito pamoja na fedha zinazotengwa kwa ajili ya kuboresha huduma za lishe kwenye Halmashauri kwa watoto wa chini ya miaka mitano.
Aidha katika kikao hicho Mkoa umeazimia kuimarisha usimamizi shirikishi ngazi ya Mkoa na Halmashauri za wilaya kwa wahudumu wa Afya ngazi ya jamii pamoja na kushauri Wakurugenzi wa Halmashauri za Wilaya Kutenga ama kuongeza kiasi Cha fedha kinachotengwa kwa ajili ya kutumika katika afua za lishe kwa watoto chini ya miaka mitano.