Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere - Mara

HOSPITALI YA RUFAA YA MKOA YA KUMBUKUMBU YA MWL NYERERE-MARA IMEANZA KUTOA MATIBABU YA WATOTO WENYE CHANGAMOTO YA VICHWA VIKUBWA NA MGONGO WAZI

Posted on: August 16th, 2024

Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere imeanza kutoa matibabu ya watoto wenye changamoto ya vichwa vikubwa na mgongo wazi baada ya kukamilika kwa mafunzo yaliyotolewa na Madaktari Bingwa wa Upasuaji wa Ubongo na Mgongo kutoka Hospitali ya Kanda Bugando Mwanza.

Akizungumza wakati wa Mafunzo hayo Daktari Bingwa wa upasuaji wa ubongo na mgongo kutoka Hospitali ya Kanda Bugando Mwanza Dkt. Gerald Mayaya amesema lengo kuu ni kuwawezesha timu ya upasuaji ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Kumbukumbu ya Mwl Nyerere waweze kuwatibu hawa watoto.

“Lengo kubwa la haya mafunzo ni kuwawezesha Madaktari hawa waweze kuwahudumia hawa watoto wa Mkoa Mara Mfano kwa Bugando tunaona watoto 700 kwa mwaka laikini kati ya hao watoto 50 wanatokea Mkoa wa Mara na karibia asilimia 70% wamekuwa wanachelewa matibabu kwahiyo sasa tumeamua kuja kuwajengea uwezo Madaktari hawa ili kuwahudumia na itasaidia kupunguza rasilimali muda na fedha” Amesema Dkt Mayaya

Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya Upasuaji ambaye pia ni Daktari Bingwa wa Upasuaji Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Kumbukumbu ya Mwl Nyerere Dkt Lesso Mwinyimkuu amesema kuwa kupitia mafunzo haya watawaongezea ujuzi ambao utawasaidia wakati wa matibabu ya watoto wenye changamoto ya vichwa vikubwa na mgongo wazi.

Vilevile, Dkt Lesso ametoa wito kwa wananchi wa Mkoa wa Mara kuwaleta watoto wao ambao wana changamoto hizo ili waweze kupata matibabu.

Kwa upande wakenMkurugenzi wa Mwanangu Development Tanzania Bw. Walter Miya amesema lengo la kutoa mafunzo haya kwa Hospitali za Rufaa za Mikoa ni kuhakikisha wanawajengea uwezo Madaktari ili waweze kutoa huduma hiyo, huku baadhi ya wananchi walionufaika na huduma hiyo wamepongeza kwani imesaidia kuboresha na kupunguza umbali mrefu na kuokoa Maisha ya watoto wao.