Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere - Mara

GRAPH YA UCHUNGU ILIYOBORESHWA NDIYO NYENZO KUU INAYOMUONGOZA MTOA HUDUMA KATIKA MAENDELEO YA MAMA ALIYEPO KWENYE UCHUNGU

Posted on: March 6th, 2024

Bw, Bahati Katembo ambaye ni Mkunga Mbobezi na msimamizi wa mafunzo ya Graph ya uchungu kutoka Hospitali ya Benjamin Mkapa Jijini Dodoma amesema kuwa Graph ya uchungu iliyoboreshwa ndiyo nyenzo kuu inayomuongoza mtoa huduma katika maendeleo ya mama aliyepo kwenye uchungu hadi pale atakapo jifungua salama.

Ameyasema hayo Machi 6, 2024 katika hitimisho la mafunzo ya graph ya uchungu iliyoboreshwa katika maswala ya uzazi kwa watoa huduma za afya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere-Mara.

Bw, Bahati Katembo amesema kuwa mafunzo haya yamekuwa muhimu sana kwa watoa huduma za afya hususani katika maswala ya uzazi.

“Mafunzo haya yamekuwa muhimu sana hasa kwa watoa huduma za afya hususani katika maswala ya uzazi kwasababu ndiyo nyenzo kuu inayomuongoza mtoa huduma katika maendeleo ya mama aliyepo kwenye uchungu had pale atakapo jifungua salama” Amesema Bw, Bahati Katembo

Aidha, Bw, Bahati Katembo ameongezea kuwa mafunzo haya yamekuwa na faida kubwa kwasababu yametoa miongozo kwa mtu wa kuambatana na mama aliyekuja kujifungua kuwa nae kuanzia mwanzo wa uchungu hadi pale atakapo jifungua na hiyo inasaidia mama aliyekuja kujifungua ajisikie yuko huru kwa kuwa na ndugu yake wa karibu zaidi ambaye amemchagua.

Kwa upande wake Muuguzi Mkuu wa Mkoa wa Mara Bw, Stanley Kajuna amesema kuwa shabaha kubwa ya kutoa mafunzo haya ni kuwajengea uwezo watoa huduma katika wodi za wazazi ili kuendelea kutoa huduma Bora.

“ Shabaha yetu kubwa kutoa mafunzo haya ni kuwajengea uwezo watoa huduma katika wodi hizo za wazazi ili kuendela kutoa huduma sahihi na bora kwa kila mama anayejifungua tunachokitarajia mafunzo haya yatawapa morali na uwezo wa kutambua vidokezo vya hatari na kuendelea kumfatilia mama wakati wote wa uchungu” Amesema Bw, Stanley Kajuna

Mafunzo haya yalikuwa ya siku tatu ambayo yalianza tarehe 04/03/2024 na kuhitimishwa siku ya jana ya tarehe 06/03/2024 ambapo jumla ya watoa huduma 11 wamepata mafunzo na kati yao mmoja ni Daktari na 10 ni wauguzi. Pia mafunzo haya yaliambata na mafunzo kwa vitendo.