Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere - Mara

CHANJO YA UVIKO- 19 NI SALAMA

Posted on: August 9th, 2021

Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara kupitia Kitengo cha Magonjwa ya Ndani Leo tarehe 8 Agosti 2021 imetoa mafunzo kuhusu Usalama na Ufanisi wa Chanjo ya Uviko – 19 kwa watumishi wake ikiwa na lengo la kuhakikisha watumishi wa afya wanakuwa na elimu na uelewa yakinifu kuhusu chanjo ya Uviko 19 inayoendelea kutolewa nchini kote.

Akizungumza wakati wa mafunzo hayo Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara Dkt. Joachim Eyembe amewataka watumishi wa Afya kuondoa hofu na kutumia fursa hii adhimu ambayo serikali imewapatia kuchoma chanjo hii  kwani ni salama na haina madhara yeyote kwa binadamu.

“Chanjo hii ni salama na niwaombe wote kwa hiari zetu tuchanje kwani inasikikitisha kuona sisi watumishi wa afya ambao ndio wenye wajibu wa kutoa elimu na kuhamasisha jamii kutambua umuhimu wa chanjo  hii tukiwa bado hatujachanja”amesema dkt Eyembe.

Aidha amewataka Wataalamu wa Afya kuendelea kutoa elimu kuhusu chanjo hiyo ili wananchi waweze kupata uelewa, kutambua umuhimu wa chanjo na kuweza kuchanja kwa hiari yao wenyewe.

“Ndugu zangu wote tunatambua ugonjwa  huu upo,na katika hospitali yetu pia tunao wagonjwa na wengine tunawapoteza ikiwemo ndugu zetu na  wataalamu wenzetu wa Afya,kwa hiyo niwasihi tuchanje na tutoe elimu kwa wananchi wachanje na kuendelea kuchukua tahadhari zote za kujikinga”amesema dkt Eyembe

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mara Dkt.Juma Mfanga ameupongeza Uongozi wa Hospitali kuchukua hatua hiyo ya kuwajengea uwezo watumishi wake kwani wao ndio wanapaswa kuwa mstari wa mbele kuelimisha  jamii kuhusu chanjo hii.

“Watumishi wa afya  wakiwa na uelewa wa kutosha kuhusu chanjo hii itawasaidia kutoa elimu  inayostahili kwa jamii na kuwaondolea hofu waliyonayo kutokana na maneno ya uzushi yaliyopo mtaani kwamba chanjo hii si salama na inaleta madhara kwa binadamu”alisema dkt. Mfanga.

Aidha amewaasa watumishi wa Afya pamoja na wananchi kuacha tabia ya kuugulia nyumbani pindi wapatapo dalili za Uviko - 19 badala yake wafike katika kituo cha kutolea huduma za afya na kupata ushauri wa kitaalamu kwani kwa kufanya hivyo kutasaidia kupunguza adhari zitokanazo na kuchelewa kupata huduma za matibabu.

Aidha amewataka watumishi kuendelea kuchukua tahadhari za kujikinga katika maeneo yao ya kazi ikiwemo kuvaa barakoa,kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni,kutumia vitakasa mikono pamoja na kuendelea kufuata miongozo mbalimbali inayotolewa na Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto kuhusu kujikinga na UVIKO 19.